Nyerere katika kesi ya uchochezi 1958

*Kuelekea kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Nyerere tunapitia kesi aliyoshtakiwa kwa uchochezi mwaka 1958. Wengi waliamini kwamba matokeoa ya kesi hiyo yangezima kabisa ndoto zake za kuongoza mapambano ya ukombozi kupitia Tanganyika African National Union (TANU).*

*Tunatazama timu ya wanasheria wa Nyerere wakiongozwa na Dennis Pritt walivyowabana mashahidi wa serikali ya kikoloni.*

Mwandishi wa Makala hii ni Mwalimu Evaristy Masuha

0717697205 

Masuha8@gmail.com 

*Sehemu ya ushahidi ni dhidi ya MJ. Macknley, Kamishina msaidizi wa Polisi.*

Pritt. “Siku ya kwanza ulipekua ofisi ya TANU kwa warrant yako, siku ya pili ukapekua jengo hilo kwa warrant ile ile ya jana yake. Je, ndivyo sheria inavyosema”?

*Macknley.* Hapana, sheria haisemi hivyo.

*Pritt:* Unakubali ulifanya makosa?

*Macknley.* ndiyo nakubali kosa.

*Pritt.* Unaheshimu sheria?

*Macknley.* Ndiyo naheshimu sheria.

*Pritt:* Asante.

*Utangulizi wa historia ya Kesi*

Julai 7 mwaka 1958 ilikuwa ni sikukuu ya Sabasaba, Kumbukumbu ya kuzaliwa kwa chama cha TANU. Kama ilivyokuwa kila mwaka. Sabasaba hii ilikuwa tofauti kabisa na sabasaba zote zilizowahi kutokea katika historia ya sikukuu hizo katika taifa la Tanganyika. Ni sikukuu iliyofuatiliwa kila kona ya Tanganyika.

Siku hiyo ilitarajiwa Mwenyekiti wa TANU Mwalimu Julius kambarage Nyerere alihutubie Taifa. Siku mbili baada ya Hotuba hiyo, Tarehe 9/07 Mwalimu Nyerere alitarajiwa asimame kizimbani kujibu tuhuhuma za uchochezi, Wafuasi wake  waliamini matokeo ya kesi hii ni hukumu ya kifungo cha muda mrefu hali ambayo itadhoofisha kabisa harakati za ukombozi.

Kesi hiyo ilikuwa imefikishwa mahakamani Juni 9, 1958. Ikapewa namba 2207/58 ikapangwa isikilizwe kuanzia tarehe 9 Julai, 1958.

Kabla ya julai 7, 1958 magazeti yote Tanganyika yaliandika yakitabiri nini kitatokea wakati na baada ya hiyo hotuba. Wasomi na wachambuzi wenye mlengo wa ukombozi kwa taifa la Tanganyika walitoa maoni yao wakishauri nini kifanyike, nini aongee ili nchi iendelee kuwa na amani lakini iwe ni karata ya mafanikio kwa TANU.

Wenye misimamo ya ubabe walishauri Nyerere ‘amwage Mboga’ wakiamini Serikali ya Kiingereza iliyokuwa ikitawala Tanganyika tayari ilikuwa ‘imemwaga ugali’. Hawa walitaka Nyerere ahamasishe vurugu ili tarehe 9 wakati wa kusikilizwa kesi taifa lisikalike.

Wenye mawazo ya kuiamini haki mbele ya sheria wakaendelea kuwa washauri wakimtaka Nyerere aendelee kutangaza na kuhamasisha amani. Mazungumzo yake yasiingilie shauri ambalo tayari lilikuwa mahakamani.

Katika makanisa mbalimbali likiwemo kanisa Katoloki ambalo mwalimu Nyerere alikuwa mmoja wa waumini wake wakaendedelea kuhubiri amani, wakimuombea na kusisitiza maandiko matakatifu yanayomtaka anayepigwa shavu la kushoto, ageuze na la kulia. Mkutano huo wa Sherehe za Sabasaba ulipangwa ufanyike katika uwanja wa Uhuru wa sasa. Zamani zile ukiwa ni uwanja wa Ndege.*

Kesi ya Mwalimu Nyerere ilitokana na Makala yake kwenye gazeti la ‘Sauti ya TANU’  toleo namba 29  lilillochapishwa Mei 7, 1958 ambalo tafsiri ya serikali ya kikoloni, makala hiyo ililenga kuchochea wananchi waipinge serikali halali iliyokuwepo madarakani.

Ikumbukwe kwamba wakati huo TANU ilikuwa katika mapambano ya kudai uhuru wa Tanganyika kutoka kwa waingereza ambao walikuwa wamekabidhiwa koloni hili kwa ajili ya kulisimamia. Chama cha TANU         kiliamini kuwa badala ya waingereza kuiandaa Tanganyika kujitawala, walikuwa wakipambana kuhakikisha wanaendelea kutawala na kunyonya rasilimali za Tanganyika.

Mashtaka ya Nyerere yalikuwa matatu. Kwanza kumkashifu Mkuu wa Wilaya ya Musoma, DC Weeks, Pili kumkashifu Mkuu wa Wilaya ya Songea, DC Scot. Tatu kuwakashifu kwa pamoja Wakuu hao wawili wa Wilaya. Wakili Dennis Pritt alikuwa kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi na alitarajiwa kuwepo kwenye Jukwaa la sherehe za Sabasaba.

Uraia wa Pritt alikuwa ni mwingereza. Kesi ya Nyerere na Mwenyekiti wa TANU ilikuwa dhidi ya Serikali ya Uingereza. Hata hivyo hakuna aliyekuwa akitilia shaka nia ya dhati ya Pritt kuhakikisha Nyerere na chama chake wanaendelea kuwa huru katika kazi zao.

Kabla ya kujitosa katika kesi hii tayari Pritt alikua na historia nzuri ya kutetea haki hasa kwa nchi ambazo zilikuwa katika mapambano ya kudai uhuru. Moja ya kesi iliyokuwa imempa sifa kubwa ni kesi dhidi ya Kenyata na wenzake wakituhumiwa kuanzisha na kuendesha jeshi la Maumau hapo Kenya.

Kama ilivyokuwa kwa Tanganyika, hapo Kenya Pritt alikuwa akipambana na serikali ya Uingereza na aliifanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa ambayo yamesababisha leo hii moja ya barabara huko Nairobi kupewa jina lake ‘Denis Pritt Road.’

Sifa nyingine ya Pritt alikuwa ni mwanasiasa wa chama cha siasa cha Labour cha huko Uingereza ambaye amewahi kuwa mbunge kupitia chama hicho mwaka 1935 akiongoza jimbo la Hammersmith North.

Kuelekea Mkutano huo na hasa kuzingatia umuhimu wake maandalizi yalikuwa mengi. Taarifa za siri za TANU zilitilia mashaka uwezekano wa serikali kuhujumu tukio hilo ikiwemo kutega mabomu.

wananchi waliamini Nyerere anaonewa na kwamba kuna njama za kumhujumu kwa hiyo walikuwa wakijipanga kwa mbinu mbalimbali. Baadhi ya mambo yaliyokuwa yakitoa tafsiri ya hila katika kesi hiyo ni pamoja na mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na serikali ya Uingereza wakati kesi ya Nyerere ikiendelea. Gavana wa koloni la Tanganyika Edward Twining alibadilishwa, akaletwa Richard Turnibal akitokea Kenya ambako vita ya MauMau ilikuwa ikirindima.

Kutokana na msuguano uliokuwepo kati ya Nyerere ya Twining wengine walihisi ni fursa ya kesi ya Nyerere kwenda vizuri. Wengine wakihisi Turnibal ameletwa kimkakati ili kuwamaliza wanasisa wa Tanganyika hasa wale wa chama cha TANU. Hili lilizungumzwa sana kutokana na kwamba kesi ilianza tarehe 9 Julai mwaka 1958, Gavana mpya, Richard Turnibal akawasili Tanganyika Julai 14 wakati kesi ikiendelea kusikilizwa.

Ujio huo ukaibua maandiko mbalimbali kwenye magazeti likiwemo gazeti la Mwafrika ambalo liliandika kichwa cha habari ‘Secretary wa Maumau, Gavana Tanganyika.’

Mwandishishi wa kitabu ‘Kesi ya Mwalimu Nyerere 1958’ kilichoandikwa na mmoja wa waandishi wa habari wa gazeti la Mwafrika, Simon Ngh’waya na ambaye wakati huo alikuwa mwandishi wa gazeti hilo anakili kwamba kwenye kikao cha ukaribisho na utambulisho wa Turnibal, Turnibal alitamka wazi kutoridhishwa na kichwa cha habari cha gazeti hilo. Alisema yeye siyo gazana wa Maumau bali amekuja Tanganyika kusaidiana katika kujenga nchi katika kipindi hicho cha mpito ambacho wanaliandaa taifa kupata uhuru. Gazeti la Mwafrika lilikuwa moja ya magazeti yaliyokuwa na mlengo wa ukombozi yakisaidia harakati za TANU.


Makala hii imeandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali pamoja na kitabu cha Kesi ya Julius Kambarage Nyerere 1958. kilichoandikwa na Simon Ngh'waya

Itaendelea…


Kuelekea siku ya mkutano hamasa ya wazi na ya siri iliendelea kusisitiza kuimarisha ulinzi. watu walisisitizwa wasiwashe moto wala kuvuta sigara katika eneo la mkutano kwa kuhofia kuchochea kulipuka kwa mabomu iwapo yatakuwa yametegwa maeneo hayo. 

Awali mikutano ya TANU ilikuwa ikifanyika kwenye uwanja wa Mnazi mmoja. Baada ya kubaini kuwa uwanja huo unazidiwa na idadi ya watu wanaokuja kusikiliza mikutano, ikakubalika shughuli hizo wazihamishie uwanja wa Taifa.

Kwa ujumla wakati huo kulikuwa hakuna mtu wa kukizuia chama cha TANU kutokana na mwitikio mkubwa wa watu, na mapenzi makubwa ya watu kwa kiongozi wao mwalimu Julius kambarae Nyerere.

Siku ya Mkutano ilifika. Watu wengi wakahudhuria. Wengi wakitamani kupata maelekezo ya nini cha kufanya ili kuhakikisha kiongozi wao anaendelea kuwa salama.

Muda wa kuhutubia mwalimu Nyerere ulifika. Kama kawaida ya mwalimu Nyerere alisimama kwa bashasha, akatoa salam na kuwashukuru wanachama wa TANU na wananchi wote wa Tanganyika. Tofauti na matamanio ya waliohitaji Nyerere ahamasihe vurugu za kuvunja amani, sehemu kubwa ya mazunguzo yake ikawa kusisitiza amani na umoja kwa wananchi na wanachama wote wa TANU.

“Tulieni kimya kesho kutwa wakati kesi yangu itakapokuwa inaendelea. Chungeni. Silaha yetu kubwa ni umoja. Ifanyeni keshokutwa kuwa ni siku kubwa sana katika jitihada zetu za kudai uhuru. Tulieni kimya hata kama mtachokozwa. Mashtaka yangu haya ni hatua nyingine kubwa ya kuendeleza mbele mapambano yetu.”

Alisema Nyerere huku akiendelea kusisitiza kuwa hakuna nchi hata moja duniani iliyojipatia uhuru wake bila kuupigania na kuutolea jasho hivyo wawe tayari kwa mapambano na wasikate tamaa.

Akagusia mapambano yaliyokuwa yakiendelea katika nchi zingine za kiafrika na kwamba hawako peke yao. Akavitaja vita iliyokuwa ikiendelea huko Algeria ambako Ben Bella alikuwa akiwaongoza waafrika wenzake kudai uhuru wa Algeria. Akayataja mapambano ya Ghana chini ya Nkwame Nkurumah yalivyowezesha uhuru wa Ghana mwaka 1957.

Akazungumzia moto wa TANU ulivyosambaa na kuwavutia wengi. Akaitaja barua iliyoandikwa na uongozi wa chama cha United Tanganyika Party (UTP) kwamba wameomba waungane na TANU lakini TANU haiko tayari kuungana nao kwa sababu chama hicho hakina nia ya dhati ya mapambano ya uhuru wa Tanganyika. Kinataka kuendelea kutawaliwa na wazungu. Chama hicho kilikuwa kimeanzishwa na mzungu Ivon Beydon na baadaye Sheikh Hussein Juma wakati huo makao yake makuu yakiwa Tanga.

Muda wote wa hotuba Nyerere alikuwa akishangiliwa na umati mkubwa wa watu. Alipotaja kukataa kuungana na UTP shangwe zikawa kubwa. Kelele za tuko pamoja zikawa kubwa. Mkutano ukaisha. Nyerere akaondoka na makamu wake John Rupia, watu wakabaki wakijipanga namna ya kuhudhuria mahakamani kusikiliza kesi hiyo.

Siku ya kusikilizwa shauri iliwadia. Mwenendo wa kesi ulikuwa ukifanyika kwa kiingereza, lugha ambayo wanachama wengi wa TANU walikuwa hawaijui. Siku ya kesi mahakama ilifurika ndani na nje. Ulinzi uliimarishwa kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.

Hakimu aliingia kisha mwendesha mashtaka akamuita Nyerere kizimbani. Kitu ambacho hakikutarajiwa na ambacho si kawaida ya mahakama wasikilizaji karibia wote ukumbini walisimama, wakainua mikono yao juu na kutamka neno ‘Uhuru’.  Ilitarajiwa Nyerere ajibu ‘na umoja’, lakini aliwatazama akakaa kimya kutii taratibu za Mahakama. Hali ikaendelea kuwa shwari.

Mashtaka yakaanza kutajwa kwa lugha ya kiingereza huku wengi wakitazama uso wa Nyerere kubaini nini kinachoendelea.

Nyerere alionekana mchangamfu kama kawaida huku wakili wake Dennis Pritt akionekana kulimudu jukwaa pamoja na wanasheria wenzake wa utetezi,  mahamoud rattansey pamoja na K.L Jhaveri.

Hakimu alikuwa L.A Davies wakati mwanasheria wa serikali na kiongozi wa mashtaka alikuwa J.C Summerfield. Shahidi upande wa serikali alikuwa F.B weeks ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma pamoja na G.T.C Scott ambaye alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Songea

Pritt alianza kuonesha umahiri wake katika maswali kwa polisi aliyetumwa kwenda kupekua ofisi za Sauti ya TANU kwa lengo la kupata Ushahidi wa uchochezi alioufanya Mwalimu Nyerere.  Sehemu ya maswali Pritt alitaka kujua iwapo alitumia Kibari cha ukaguzi (warrant) maalumu inayomruhusu kukagua akasema ndiyo, akamuuliza iwapo siku ya pili pia alipoenda kukagua ofisi ya TANU alitumia warranti hiyo hiyohiyo. Akasema ndiyo. Akamuuliza iwapo alichukua baadhi ya vitu kutoka ofisi ya TANU, akasema ndiyo.

“Siku ya kwanza ulipekua ofisi ya TANU kwa warrant yako, siku ya pili ukapekua jengo hilo kwa warrant ile ile ya jana yake. Je, ndivyo sheria inavyosema?”

Hapana, sheria haisemi hivyo.

Unakubali ulifanya makosa?

 ndiyo nakubali kosa.

Unaheshimu sheria? 

Ndiyo naheshimu sheria.

Pritt akashukuru na kurudisha kwa hakimu aendelee na maelekezo ya kesi.

Jopo la watetezi wakiongozwa na Pritt liliendelea kuwataka serikali wawalete hao Wakuu wa Wilaya wanaodai kuwa wamekashifiwa ili wahojiwe mahakamani hapo iwapo kweli yaliyoandikwa kwenye gazeti siyo halali na kama ni kashfa na uchochezi. Mawakili wa mashtaka wakakataa kuwaleta watu hao japo awali walionesha nia ya kuwaleta.

Aidha wakati kesi inaendelea ikatokea gazeti la serikali likatangaza mabadiliko yaliyofanywa na serikali ambapo aliyekuwa chifu Musoma alihamishwa kwenda Songea.

Chifu huyu alikuwa moja ya mashahidi wa Nyerere ambaye alikuwa akilalamika kufukuzwa kazini kinyume na utaratibu. Alikata rufaa akashinda, akiwa njiani kutokea Dar es salaam kwenda Musoma alizuiwa kupande meli kutokea Mwanza kwenda Musoma. Wakati bado ameshikiliwa hapo Mwanza serikali ikatangaza kwamba amehamishwa kituo kutoka Musoma kwenda Songea. Aidha amechaguliwa Chifu mwingine wa kizungu kushikilia nafasi hiyo hapo Musoma.

Jopo la Utetezi likaiomba mahakama iwaite Mwendesha mashtaka na wote waliohusika katika uhamisho huo waje mahakamani kujibu mashtaka kwa sababu mabadiliko hayo yamefanya mashahidi wa upande wao ambao hawajatoa Ushahidi kuhofia kutoa Ushahidi kwa sababu ya yaliyomkuta mmoja wa mashahidi hao.

Baada ya hoja za utetezi kuwa na nguvu zaidi mwanasheria Mkuu wa Sekali akajitokeza mahakamani akitetea kwamba kilichoandikwa na gazeti la serikali kuhusu uhamisho huo ni taarifa kutoka serikalini. Aidha mabadiliko hayo hayakulenga kuwanyima watu uhuru.

Mvutano ukawa mkali mahakamani. Jopo la utetezi likaamua kufunga kesi na kuacha kuwaita mashahidi wengine. Wakadai haki haitatendeka. Tayari watu wametiwa hofu. Pritt na jopo lake wakaazimia kwenda mbele zaidi iwapo haki haitatenda.

Siku ya kusomwa hukumu ikawa na mvuto mkubwa kwa watanganyika wengi. Hakimu akaanza kusoma hukumu. Licha ya wananchi wengi waliojazama mahakamani hapo kutokufahamu lugha ya kiingereza iliyokuwa ikitumika katika mwenendo mzima wa kesi, tabasamu la Nyerere na shangwe za wachache waliojua lugha ya kiingereza zilitoa majibu kwamba Nyerere ameshinda, umati mzima maeneo ya viwanja vya mahakama vikapiga kelele, wakapaza sauti ya shangwe kubwa wakimshukulu Mungu kwa kiongozi wao kuwa huru.

Nyerere akahukumiwa kulipa faini ya shilingi 3,000 au kifungo cha miezi 6 jela. Chama cha TANU kikalipa fedha zote, Nyerere akawa huru. Harakati za ukombozi zikaendelea.

Kwa mjibu wa mwandishi Simon Ngh’waya katika kitabu chake cha ‘Kesi ya Mwalimu Nyerere 1958’ Pritt alilipwa jumla ya shilingi 23000 kama gharama za kazi yake ya Uwakili katika kesi hiyo.

Sehemu kubwa ya Makala hii imeandikwa kwa kutumia kitabu cha Kesi ya Mwalimu Nyerere 1958 kilichoandikwa na mmoja wa waandishi wa habari wa gazeti la Mwafrika Simon Ngh’waya

 

Masuha8@gmail.com

0717697205

 

 

 

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

Ujenzi wa Mabwawa kusaidia kuondoa changamoto ya maji Dodoma

Wataalamu Sekta ya maji shirikishaneni maarifa – Naibu Waziri Maji

Katibu Mkuu Wizara ya Maji asisitiza matumizi ya mfumo wa taarifa za sekta ya maji (Maji App)