Katibu Mkuu Wizara ya Maji asisitiza matumizi ya mfumo wa taarifa za sekta ya maji (Maji App)


Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amewataka wataalam wa sekta ya maji kuhakikisha wanahuisha takwimu na taarifa mbalimbali kwenye mfumo unaotoa taarifa za sekta ya maji, Maji Mobile Application (Maji App) ili kuendana na mabadiliko ya kila siku.

Mhandisi Sanga amesema mfumo huo ulizinduliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 22, 2022 kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa za sekta ya maji kwa wakati. Ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha wataalam wanaojenga mifumo na masuala ya takwimu katika sekta ya maji jijini Dodoma leo.

Wataalamu wa sekta ya maji katika kikao kuhusu takwimu na mifumo ya kieletroniki 

Ameongeza  kuwa kwa muda mrefu sekta ya maji imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa takwimu sahihi, zenye ubora na kwa wakati. Pia kuwepo kwa  mifumo ya kielektroniki katika Idara za Wizara na Taasisi zake ambayo ilikuwa haiongei pamoja.

Mhandisi Sanga amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Sekta ya Maji (Integrated Water Sector Monitoring and Evaluation System – IWSMES) pamoja na mifumo mbalimbali ya kielektroniki ikiwemo Maji App kwa lengo la kukusanya, kuchakata na kutoa takwimu za miradi ya maji, wataalamu wanalo jukumu la  kuhakikisha taarifa zinawekwa  kwa wakati.

Picha ya pamoja Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kutoka kulia waliokaa) pamoja na wataalam waliobuni na kutengeneza mifumo ya Taarifa za sekta ya maji (Waliosimama nyuma)  

Kikao kazi hicho kimebeba kaulimbiu isemayo “Matumizi ya Maji App kwa Takwimu Sahihi” na kimejumuisha zaidi ya wataalam 260 wanaohusika na mifumo pamoja na  takwimu katika sekta ya maji kutoka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ; Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira, na miradi ya maji ya kitaifa; Bodi za Maji za Mabonde na Maabara za Ubora wa Maji.

 

 

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

Ujenzi wa Mabwawa kusaidia kuondoa changamoto ya maji Dodoma

Wataalamu Sekta ya maji shirikishaneni maarifa – Naibu Waziri Maji