Mto Mara: Kiungo cha Maisha Yetu, Urithi Wetu
Kwa familia nyingi, Mto Mara ni maisha. Unanywesha mifugo , unawasaidia kwenye kilimo, na unawawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku. Kwa watoto, mto huu ni darasa la asili wanajifunza kuogelea, kuvua samaki, kuwaona ndege na miti ya asili. Kwa watalii wanaomiminika kila mwaka Serengeti, ni jukwaa la kushuhudia maajabu ya dunia: Nyumbu na Pundamilia maelfu wakivuka maji kwenda Kenya.
Ni nyumbu hao
ambao wanatajwa kwenda nchini Kenya ambako wanaanzisha mahusiano ambayo
yanazalisha mimba, kisha wanavuka kurudi Tanzania kuzaa na kuanza malezi ya watoto.
Mto
Mara unapita katika nchi mbili: Kenya na Tanzania. Unaanzia katika Safu ya
Milima ya Mau nchini Kenya, unapitika kwenye Hifadhi ya Wanyamapori ya
Maasai-Mara nchini Kenya na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania,
hatimaye kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria.
Mto huu umekuwa kiungo cha
ushirikiano wa mataifa ya Tanzania na Kenya, ukiimarisha Diplomasia ya Uchumi, mshikamano
wa kijamii na kitamaduni. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan, mara kwa mara amesisitiza umuhimu wa kuyatumia maji kama
chachu ya kudumisha mahusiano ya kikanda na kimataifa.
Kwa mwaka huu wa
2025 kuanzia Septemba 13–15, mataifa haya yanayounganishwa na Mto
Mara yatakutana mjini Butiama, chini ya kaulimbiu “Hifadhi Mto Mara: Linda
Uhai.” Haya si maadhimisho au sherehe tu. Ni nafasi ya watu kujiuliza
swali muhimu: Kama sisi ttulivyourithi, tutauachaje mto huu kwa vizazi
vijavyo?
Maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mto
Mara, yanaandaliwa kwa ushirikiano kati
ya Wizara ya Maji na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Septemba 15 imekuwa ikiheshimiwa
kila mwaka kama Siku ya Mto Mara, ikihusiana moja kwa moja na tukio la kihistoria
la msafara wa nyumbu wanaovuka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tanzania,
kuelekea Hifadhi ya Maasai-Mara nchini Kenya, na kurejea tena Serengeti. Tukio
hili limekuwa kivutio kikubwa cha utalii duniani, likiibua heshima kubwa kwa
Tanzania kama kitovu cha utalii wa asili.
Mto Mara pia ni chanzo kikuu cha
maji katika Ziwa Victoria, ziwa kubwa la maji baridi barani Afrika na la pili
kwa ukubwa duniani. Maji yake yananufaisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda
kwa upande wa Afrika Mashariki, yakiendelea kusafiri hadi nchini Misri katika Bahari
ya Mediterania kupitia Mto Nile.
Chanzo cha Mto Mara ni chemichemi za
Enopuyapui katika Milima ya Mau nchini Kenya, na huchukua eneo la kilomita za
mraba 13,504, ambapo asilimia 65 ipo Kenya na asilimia 35 ipo Tanzania.
Zaidi ya kuwa mhimili wa uhai kwa
binadamu, mifugo na wanyamapori, Mto Mara umekuwa kichocheo cha uchumi kupitia
kilimo, uvuvi na utalii. Watafiti wanabainisha kuwa bila uhifadhi thabiti wa
mto huu, maisha ya mamilioni ya watu na viumbe hai katika ikolojia ya
Mara-Serengeti yangetumbukia hatarini.
Kutambua uzito huo, Serikali ya
Tanzania imeamua mwaka huu kuyaunganisha maadhimisho ya Siku ya Mto Mara na Mkutano
wa Kimataifa wa Wanasayansi wa Maji (International Maji Scientific Conference)
unaoratibiwa na Chuo cha Maji. mkutano huu utawaleta na kuwakutanisha pamoja
wataalamu kutoka duniani kote kujadili tafiti na masuala muhimu yanayohusu
maji, ili kupata suluhisho la kitaalamu.
Aidha, shughuli za upandaji miti
rafiki wa maji zimepangwa katika maeneo mbalimbali kama njia ya kulinda vyanzo
vya maji na kuimarisha uendelevu wa ikolojia. Pia, michezo na mashindano
mbalimbali yatafanyika ili kuhamasisha jamii kushiriki moja kwa moja katika
uhifadhi wa rasilimali hii adhimu.
Dkt. Masinde Bwire
wa Kamisheni ya Bonde la Mto Nile anasema Siku ya Mto Mara ni jukwaa la
kutambua na kulinda uhai wa mfumo ikolojia wa Mara-Serengeti. Ni jukwaa la
kutambua kwamba kila tone la maji lina umuhimu kwa binadamu na mnyama
anayelitegemea, Pamoja na ikoljia yote kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, Tanzania
imedhihirisha uongozi imara ndani ya Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria,
ikishirikiana na nchi Tisa wanachama ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda,
Burundi, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ushirikiano
huu umenufaisha miradi mikubwa ukiwemo ule wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa
Mazingira Mwanza (MWAUWASA)
jijini Mwanza kupitia Programu ya Pamoja ya Usimamizi na Uendelezaji wa
Rasilimali za Maji katika Bonde la Ziwa Victoria (LVB-IWRM), wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 12.6. Mradi
huu unalenga kujenga miundombinu ya majitaka na usafi wa mazingira jijini Mwanza
Rais wa Tanzania,
Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kusisitiza kuwa uhifadhi wa rasilimali za
maji ndio msingi wa mshikamano wa kikanda na ustawi wa kijamii. Ni kupitia
juhudi kama hizi Tanzania imejipambanua si tu kama taifa la hifadhi ya
wanyamapori, bali pia taifa la uhifadhi wa uhai.
Aidha, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso,
ameweka msimamo wa wazi kuwa Wizara haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote
atakayehatarisha usalama wa Mto Mara akisisitiza kuwa mto huu ni tegemeo la
maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa maelfu ya wananchi, na ndio msingi wa
mustakabali wa utunzaji wa mazingira na uhakika wa huduma ya majisafi na salama
nchini Tanzania.
Wakati watalii
wakipiga picha za nyumbu wakivuka, tumkumbuke mama wa Kijiji cha Kirumi, anayehitaji
huduma ya majisafi na salama kwa matumizi ya nyumbani, Tumkumbuke mvuvi kutoka
Kijiji cha Manga ambaye pato la familia yake linatokana na mto Mara. Tumkumbuke
Mtoto kutoka kitongoji cha Makora anayeogelea kandokando ya mto. Wote hawa
wanashuhudia kwamba Mto Mara ni zaidi ya maji, Mto Mara ni uhai.
Kwa mantiki hiyo, uhifadhi wa Mto
Mara si hiari bali ni wajibu wa kizazi chetu. Ni njia ya kulinda urithi wa
asili, kuchochea uchumi, kuzuia mafuriko na kukabiliana na changamoto za
upungufu wa maji.
Hifadhi Mto Mara: Linda Uhai.
Twendeni Mara. Twendeni Butiama.
Ni Tarehe 13-15, 2025








Comments
Post a Comment