Tanzania, Msumbiji na Malawi wasaini makubaliano ya ushirikiano Bonde la Mto Ruvuma
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) pamoja na Mawaziri wenza wanaosimamia sekta ya maji kutoka nchi za Malawi na Msumbiji wamesaini makubaliano yenye lengo la kuweka mikakati ya pamoja katika utunzaji, ulinzi na uendelezaji wa Bonde la Mto Ruvuma.
Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dar es Salaam
ambapo upande wa Malawi wamewakilishwa na Waziri wa Maji Mhe. Abida Sidik Mia
na nchi ya Msumbiji ikiwakilishwa na Waziri wa Maji Mhe. Carlos Mesquita.Katika mkutano huo Waziri Aweso amesema suala la
usimamizi wa rasilimali maji lazima liwe la pamoja ili kupambana na mabadiliko
ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakiathiri rasilimali hiyo kwa muda mrefu.
Amesema ndoto ya waasisi wa Serikali zote tatu ilikuwa ni kudumisha umoja
kizazi hadi kizazi.
“Hayati Mwalimu Nyerere alisema bila umoja hakuna
maendeleo Afrika, Hayati Samora Machel wa Msumbiji akasema ili taifa liendelee
kuwa salama lazima ukabila uondoke (For the Nation to live, the tribe must
die). Aidha hata nembo ya taifa la Malawi inaelezea Umoja na Uhuru. Mhe. Aweso
ameongeza
Aidha, Waziri Aweso amewataka wadau mbalimbali wa
maendeleo, taasisi na sekta zote kujitokeza ili kusaidia jitihada hizo
zilizoanzishwa huku akisisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko tayari kuhakikisha ushirikiano huo
unaendelelea kuimarishwa.
Kwa upande wa Waziri Sidik Mia kutoka Malawi
amesema mafanikio ya usalama wa bonde la Mto Ruvuma ni heshima kwao na vizazi
vijavyo hivyo lazima wote kwa pamoja wahakikishe kazi hiyo inafanikiwa, huku
Mhe. Carlos Mosquita wa Msumbiji akisisitiza umoja na kuwataka Wanachi na wadau
wote kutoa ushirikiano.





Comments
Post a Comment