Huduma ya maji inavyochochea Tanzania ya Viwanda Kibaha.
Mkoa wa Pwani unapakana na bahari ya Hindi. Majirani zake ni pamoja na mkoa wa Dar es Salaam ambao pia ni jiji maarufu la kibiashara hapa nchini Tanzania na ukanda wa kusini mwa Afrika. Kwa miaka ya hivi karibuni mkoa wa Pwani umekuwa na sifa ya ziada ya maendeleo ya viwanda. Zipo sababu nyingi zilizochochea haya, ikiwamo uwepo wa viwanda katika mji huo ikihusisha reli ya kisasa maarufu kama reli ya SGR ambayo inapita eneo hilo huku kukiwepo eneo la kimakakati la Bandari kavu ya Kwala pamoja na huduma ya majisafi na salama ambayo inatolewa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) mkoa wa Pwani pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Dar es Salaam (DAWASA).
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi
wa Mazingira vijijini (RUWASA) Wilayani Kibaha mkoani Pwani ni Mhandisi Debora
Kanyika ambaye anasema Serikali ya awamu ya sita imeonesha nia ya dhati
kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa kitovu cha maendeleo ya Viwanda na huduma
nyingi kupitia uwekezaji mkubwa aliowekeza Mheshimiwa Rais kupitia huduma ya
majisafi na salama.
Anasema huduma ya majisafi
wilayani hapo sasa imewafikia wananchi kwa asilimia 78 huku jumla ya miradi mitano
(5) ikiendelea kutekelezwa. Miradi hiyo itarajiwa kukamilika na kuongeza
asilimia saba (7) ya huduma na kuifanya
wilaya hiyo kufikia asilimia 85 ya huduma ya maji ambayo ni moja ya malengo
yaliyoainishwa ndani ya ilani ya Chama cha Mapinduzi inayotekelezwa kuanzia mwaka
2020 hadi mwaka 2025. Licha ya hatua hiyo, Mipango ya serikali inalenga
kuhakikisha huduma ya maji inafikia asilimia mia moja na hivyo kuondoa kabisa
changamoto ya huduma ya maji kwa wakazi wa Kibaha.
Anasema huu ni uthubutu mkubwa unaofanywa
na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua kama mpambanaji ambaye
anatambua adha kubwa wanayoipata akina mama wa Tanzania katika kutafuta huduma
ya majisafi na salama.
Mhandisi Debora anamshukuru Rais kwa
kujali wananchi wa eneo la Kibaha kwa kutekeleza miradi hiyo ambayo sasa
inawezesha huduma ya maji kuyafikia maeneo yote muhimu ya kijamii pamoja na
viwanda. Aidha anamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kusisitiza huduma hiyo isiishie
kwenye maeneo ya biashara tu bali makazi ya watu na Taasisi za Kijamii ambapo sasa Mradi wa
Kwala pekee umeweza kuzifikia Taasisi 9 katika eneo hilo.
“Mheshiwa Rais kwa kutambua
umuhimu wa maji katika maeneo haya muhimu ameelekeza RUWASA kuhakikisha tunafikisha
huduma ya maji katika maeneo hayo na kuyafanya yawe maeneo yenye kujitosheleza
kwa upande wa maji. Hilo tumelitekeleza na tunaendelea kupambana kuhakikisha
huduma ya maji inakuwa endelevu ili tusikwamishe jitihada za Rais katika nia
yake ya dhati ya kuwatumikia watanzania.” Anasema Mhandisi Debora
Anasema zaidi ya shilingi Bilioni
tano (5) zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ikiwemo miradi
sita ya Mpiji, Minazi Mikinda, Kimara
Misale, Ruvu station, Kwala na
Mwembengozi, Kwala – bandari kavu na
eneo la Uwekezaji (Dry Port na Sino Tan) pamoja na uchimbaji wa visima vitatu
katika maeneo ya masaki, Kigoda na Miyombo.
Miradi hiyo imekuwa mkombozi na
kuifanya Kibaha kuwa eneo lenye matumaini makubwa ya kukua kwa sekta mbalimbali
zinazotegemea huduma ya maji. Mtandao wa mabomba katika wilaya sasa ni kilometa
193,995 ambazo zimewezesha kusambaa katika eneo kubwa la wilaya ya Kibaha
ambayo inaundwa na tarafa mbili za Mlandizi na Ruvu zenye wakazi wapatao
123,367, hii ni kwa mjibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Mhandisi Debora anasema ili
kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa endelevu, wilaya imeajiri wataalamu
wenye weledi katika usimamizi wa miradi. Anasema Jumuia za watumia maji ni eneo
muhimu ambalo wamelipa uzito kwa sababu ndio wanaohudumia walengwa kwa hiyo wameajili
wataalamu wenye weledi na wenye elimu za kutosha kusimamia miradi.
Rose Mshana ambaye ni Mhasibu wa Chombo
cha Watumia Maji Minazi Mikinda, anasema elimu yake ni Shahada ya kwanza ya
Chuo Kikuu ambako amehitimu masomo ya Uhasibu. Anaishukuru Serikali kwa kuamua
kuajili wataalamu kwani imeongeza tija katika usimamizi na kuongeza uzalishaji
na uendelevu wa miradi. Pia imesaidia kupunguza tatizo la ajira kwa watanzania.
“Naishukuru serikali kwa kuwekeza
katika sekta hii ya maji kwani imetusaidia sisi ambao tungeendelea kuwa mtaani
bila ajira. Jumuia yetu ya watumia maji Minazi Mikinda inasonga mbele. Mapato
ya mwezi yameonngezeka. Wataalamu wa serikali wanatukagua na kuridhika na
usimamizi wetu wa miradi” anasema Rose.
Pia anatoa ushauri kwa serikali kuhakikisha
inaendelea kuajiri wataalamu katika sekta zote za maendeleo ili kuondoa
changamoto ya usimamizi na uendelevu wa miradi.
Kwa upande wake Manssoor Ally
Kisabengo, Diwani wa kata ya Kwala ulipo
Mradi wa maji Kwala ambao unahudumia Kongani ya Viwanda pamoja na bandari kavu
ya Kwala anasema kala ya mradi wa maji wa Kwala hali ya huduma katika eneo lake
ilikuwa ya shida sana.
“Mradi huu umekuwa mkombozi.
Changamoto ilikuwa kubwa, tulikuwa tukiishi kwa kununua kwenye maboza na
kuombaomba. Mradi uliokuwepo ulikuwa umechakaa sana, umechoka. Sasa shida ya
maji kwala tumesahau. Tunamshukuru Rais na serikali kwa ujumla” Anasema Diwani
Kisabengo na kuendelea kwamba sasa jamii ya Kwala imekuwa na ratiba nzuri ya
maendeleo tofauti na zamani ambapo ratiba ya kutafuta maji ilikuwa ikiharibu
mipango ya maendeleo. Aidha jitihada kubwa iliyopo sasa ni kuhakikisha
wanaunganisha maji majumbani mwao. Vijana sasa badala ya kuhangaika kutafuta
kazi ya kusomba maji, sasa jitihada ni kazi ni viwandani.
Naye Fatuma Matambi, mkazi wa
Kwala anapongeza serikali na kusema sasa jamii imependeza na kung’aa kwa sababu
ya ujio wa maji. Anasema kabla ya ujio wa mradi wa maji Kwala, ilikuwa
ikiwalazimu kununua maji shilingi mia tano kisha kuingia gharama za bodaboda
kwa shilingi elfu moja kwa kila ndoo ya maji. sasa yote hayo yamekuwa historia
kutokana na uthubutu wa dhati wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia suluhu Hassan ambaye ameamua kwa dhati kumtua mtanzania kutoka
kwenye adha ya maji.
Hatua hizi zote za Serikali
kuwafikia wananchi na wawekezaji zinabeba ule msemo wa Waziri wa Maji Jumaa
Aweso (Mb) ukiwa na mgonjwa, mihemo yake unaipata sawasawa, kwa maana Serikali
imewashirikisha wananchi na kuelewa kiu yao katika huduma muhimu ya maji.


Comments
Post a Comment