Maabara ya Isotope Dodoma katika utoaji majibu ya maji
Na;
Evaristy Masuha
Mashine ya kupimia alisia ya vyanzo vya maji (Liquid Water Isotope Analyser)
Rais Samia Suluhu Hassan
atakumbukwa kwa vizazi vingi hapa nchini kwa kuwezesha maendeleo katika sekta
mbalimbali zinazoigusa jamii na uchumi wa nchi. Wadau wa sekta ya maji
wataendelea kumkumbuka kwa jinsi alivyopambana na anavyoendelea kupambana
kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inamfikia kila Mtanzania. Ameweza
kujipambanua kama mama ambaye anafahamu adha wanayopitia akinamama wenzake
katika kutafuta huduma ya majisafi.
Rais Samia amefanya maboresho
makubwa kwenye maabara ya kukusanya takwimu za maji na kuzifanyia tafiti ili
kujua ubora wake kwa matumizi mbalimbali katika jamii, Maabara hii inaitwa ya
Isotope iliyoko Jijini Dodoma kwa sasa ni maabara bora na ya kisasa katika
ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuhusu masuala ya maji. Hatua hii inazidi
kuifanya Tanzania kuwa kinara katika maendeleo ya Sekta ya Maji, kuanzia
utafiti hadi ujenzi, kama ilivyotambuliwa na Benki ya Dunia kwa ujenzi wa
miradi inayotoa huduma kwa wananchi vijijini.
Ahadi ya Chama cha Mapinduzi
kupitia ilani iliyokubaliwa na watanzania ambayo inatekelezwa ni kuhakikisha
huduma ya majisafi inafikia asilimia 85 vijijini wakati huduma hiyo maeneo ya
mijini inafikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2025. Bila shaka kila Mtanzania
anafahamu na anashuhudia jinsi Rais Samia alivyowezesha huduma hiyo kusambazwa
kwa kasi kila kona ya nchi.
Msisitizo wa Rais Samia
haukuishia kuhakikisha huduma hiyo inamfikia Mtanzania bila kuzingatia ubora wa
huduma hasa katika suala la afya. Kwa sasa Tanzania inazo maabara 17 za ubora
wa maji. Maabara saba kati ya hizo zimepata vyeti vya ithibati ambapo zinaweza
kufanya kazi kimataifa popote pale na kutambulika . Mipango na kazi inaendelea
kuhakikisha maabara zote zinakidhi viwango vya kimataifa.
Rais Samia ameendelea kuwekeza
nguvu katika ubora wa vipimo mbalimbali vya sayansi ya maji ambavyo
vinaiwezesha serikali kufanya maamuzi sahihi katika masuala mbalimbali ya
kitaalam yanayogusa sekta ya maji.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa
Aweso (Mb) anasema chini ya utawala wa Rais Samia, serikali imeiweka Wizara ya Maji
katika ushirikiano mzuri na mataifa mbalimbali ambayo yameshirikiana na
serikali kuiwezesha maabara ya Isotope iliyoko jijini Dodoma kuwa na ubora wa kimataifa.
Anasema huko Nyuma Wizara ya
Maji ilikuwa wizara ya kero na lawama kutokana na uwekezaji mdogo, lakini sasa
wizara hiyo ina bajeti kubwa. Sehemu mojawapo ambayo imeongezwa nguvu ni bajeti
kwa ajili ya kuimarisha maabara hiyo na ya kipekee hapa nchini ambayo sasa ina
vifaa vya kisasa na bora kabisa ambavyo vinawezesha kupima ubora wa maji katika
Nyanja tofauti tofauti.
Kemia
ya kawaida ambayo inapatikana kwenye maabara nyingi Afrika Mashariki na Kati inawezesha
kufahamu kiwango cha madini yaitwayo nitrate
katika mto, maji chini ya ardhi na udongo. Maarifa hayo ndiyo yanayowawesha kufahamu
usalama na ubora wa maji lakini chanzo cha uchafuzi kinajulikana baada uchunguzi
kwa kutumia isotope ya nitrate ambayo sasa inapatikana hapa Tanzania kwenye maabara
ya Isotope iliyoko Dodoma.
Maabara
hiyo imewezeshwa kuwa na vifaa vya kisasa kabisa ambavyo vinaweza kutoa majibu
ambayo hayawezi kutiliwa shaka sehemu yoyote Duniani na kwa haraka zaidi. Vifaa
hivyo ni kama Liquid Water Isotope Analyser
ambayo inaweza kupima sampuli zaidi ya 50 kwa wakati mmoja. Ion Chromtography ambayo licha ya uwezo wake wa kupima sampuli
nyingi kwa wakati mmoja, kifaa hiki kina uwezo
wa kuchambua chembe chembe za madini katika maji kama vile anions, cations, chumvi, trace elements
na protini na kutengeneza ‘distilled
water’.
Hakuna tena ulazima wa kutuma sampuli nje ya nchi isipokuwa
nchi za nje zinakaribishwa kuleta sampuli kwenye maabara ya Isotope Dodoma ili
kufanyiwa uchunguzi. Hii yote ni mafanikio ya Rais Samia baada ya kuwekeza
nguvu na bajeti ya kutosha katika sekta ya maji.
Maeneo ambayo maji yamechafuliwa na mifugo, shughuli za
kibinadamu kama madini, kilimo na ujenzi wa miundombinu ya shughuli mbalimbali
maabara ya Isotope inatoa majibu na hivyo kuwezesha kufanya maamuzi ikiwemo kuweka
miundombinu ya kuzuia uharibifu, pia kuhamisha watu, mifugo au chochote ambacho
kitabainika kuwa ndiyo chanzo cha uchafuzi wa maji.
Tofauti na maabara nyingine
sasa hivi maabara ya Isotope ina uwezo wa kipekee wa kupima maadiliko ya tabianchi kwa
siku za nyuma na hivyo kuwezesha wataalamu na serikali kwa ujumla kutoa
mwelekeo wa siku zijazo za mabadiliko ya joto duniani, pia mahitaji ya nishati,
upatikanaji wa maji ya kunywa, na vifaa vya kutosha vya chakula.
Maabara
ya kisasa ya Isotope ya Dodoma kupitia vifaa vya kisasa kabisa vilivyopo
inaenda mbali zaidi kwa kujua jinsi maji juu ya ardhi yanavyovia ardhini na
kuhifadhiwa katika miamba inayohifadhi maji chini ya Ardhi (Aquifer). Kujua
mahusiano na mwingiliano kati ya Maji chini ya ardhi na juu ya ardhi, na
mwenendo wa Maji chini ya ardhi.
Sifa hizi na nyingine nyingi zinaifanya
wengi Kutumia lugha rahisi ambayo siyo rasmi kuitambulisha maabara hii kama
Carbon 14 ya maji. Sifa hii inatokana na utofauti wake na maabara zingine, pia
aina ya kazi zinazofanywa kupitia maabara hii. Moja ya kazi hiyo ni uwezo wake
wa kutambua umri wa maji.
Kwa kawaida maji yanapatikana chini ya ardhi na juu ya ardhi.
Sehemu kubwa ya maji chini ya ardhi chanzo chake ni juu ya ardhi sababu kuu
ikiwa ni mvua. Maji haya huvuja na kujikusanya huko chini, hatimaye kutengeneza
chanzo kingine cha maji huko chini. Maabara ya Isotope ya Dodoma ina uwezo
mkubwa wa kufahamu ni lini maji hayo yaliyoko chini ya ardhi yalijitenga na
yale yaliyoko juu ya ardhi.
Eneo
jingine ambalo sasa Wizara ya Maji inajivunia kupitia maabara hiyo ni teknolojia
iliyopo kupitia vifaa vya kisasa vinavyoiwezesha kutambua chanzo cha chumvi
katika maji chini ya Ardhi iwapo imesababishwa na mwingiliano wa maji ya Bahari,
Miyeyuko ya miamba inayopitisha maji au maji yanayovia ardhini na chumvi iliyoyeyuka
na kuvukishwa (Evaporation). Pia
kufahamu iwapo maji yanavuja kuelekea eneo lolote hasa katika mabwawa ambayo
serikali imewekeza gharama kubwa kuyajenga.
Kwa
ujumla serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia imeupiga mwingi katika
maeneo mengi ndani ya sekta ya maji. Maabara ya maji Dodoma inawakaribisha
Taasisi za watu Binafsi, serikali, vyuo vikuu Taasisi za Utafiti na hata nchi
jirani kuleta sampuli za maji ili kufanyiwa uchunguzi wa kina.


Comments
Post a Comment