Miaka mitatu ya Samia katika Sekta ya maji, takwimu zinaongea.
Na;
Evaristy Masuha.
Machi 17, 2024 Rais samia suluhu Hassan alitimiza miaka mitatu akiwa madarakani. Moja ya majukumu yake muhimu wakati anaapa kuwatumikia Watanzania ilikuwa ni pamoja kuhakikisha ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyompa ridhaa ya uongozi kwa Watanzania inatekelezwa.
Upande wa Sekta ya Maji ilani
hiyo inaitaka serikali kuhakikisha wananchi wanaoishi vijijini wanafikiwa na
huduma ya maji kwa asilimia 85 wakati wale waishio mijini wanafikiwa na huduma
hiyo kwa asilimia 95. Waswahili wana msemo usemao ‘Ada ya mja hunena, muungwana
ni vitendo’. Rais Samia amedhihirisha hayo kwa vitendo kupitia uungwana wake wa
kuhakikisha ilani ya CCM hasa upande wa Sekta ya Maji inatekelezeka.
Hizi hapa ni sehemu ya
takwimu kutoka Wizara ya Maji zinazoonesha jinsi serikali anayoiongoza ilivyopiga
hatua katika kuhakikisha huduma ya majisafi inamfikia kila Mtanzania, awe mjini
au kijijini.
Takwimu kutoka Wizara ya maji kama zilivyowasilishwa
wakati wa wiki ya maji, hadi Desemba
2023 Upatikanaji wa huduma za maji ulikuwa umefikia wastani wa asilimia 84.8
ambapo kwa mjini ni wastani wa asilimia 90 na vijijini ni wastani wa asilimia 79.6.
Matumaini ya kufikia kiwango kilichoagizwa na serikali kiko wazi kutokana na
jitihada mbalimbali zinazoendelea.
Jukumu la kutoa huduma ya majisafi na salama kwa Watanzania walioko vijijini linatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). Idadi ya vijiji vilivyopata huduma ya maji hivi sasa vimefikia 9,259 kati ya vijiji 12,318 vilivyopo. Vijijiji 3,059 ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo, jitihada ziko wazi na kazi inafanyika. Matumaini ya miradi ya maji kuvifikia vijiji hivi ni makubwa kutokana na utayari wa Serikali kupitia viongozi na watendaji mbalimbali wa Sekta ya Maji.
Serikali ya Rais Samia inaendelea kutekeleza jumla ya miradi ya maji 1,790 ikiwemo 244 ya mijini na miradi 1,546 ya vijijini.
Nia ya serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwa wazi katika kuhakikisha inatumia vyanzo ya uhakika vya maji ikiwemo maziwa, mito na mabwawa kutekeleza miradi mikubwa. Baadhi ya miradi mikubwa ya maji inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na mradi wa maji wa Same -Mwanga-Korogwe, Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Katika Mkoa wa Simiyu, Mradi wa Mugango-Kiabakari-Butiama, Mto Kiwira -Jijini Mbeya, Mradi wa maji wa Miji 28, Mabwawa ya Kidunda na Farkwa na ukamilishaji wa mradi wa Arusha.
Kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha huduma ya majisafi kufikia wastani wa asilimia 85 kwa upande wa vijijini na wastani wa asilimia 95 kwa maeneo ya mijini ifikapo 2025. Aidha, eneo la usimamizi na utunzaji wa vyanzo vya maji limepewa kipaumbele kwa kuhakikisha kila mwananchi anashiriki kikamilifu ili nchi iwe na rasilimali za maji endelevu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kuanzia mwezi
Januari 2023 hadi Desemba 2023 jumla ya miradi ya maji 506 ilikamilishwa
ikiwemo 436 ya vijijini na 70 ya mijini yenye uwezo wa kuhudumia wananchi
5,754,340 (3,145,645 wa vijijini na 2,608,695 wa mijini).
Ili kuhakikisha Wizara ya Maji
inakuwa na vifaa vya kutosha katika utekelezaji wa miradi, Serikali ilinunua
mitambo ya uchimbaji wa visima, seti 25 na seti tano za mitambo ya ujenzi wa
mabwawa ambapo jumla ya visima 1,097 vitachimbwa katika maeneo mbalimbali na
mabwawa 69 yatajengwa ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi ya kijamii
na kiuchumi.
Eneo la Rasilimali za Maji pia limepewa kipaumbele. Wizara
ya Maji inayo idara mahususi yenye kazi ya kuhakikisha rasilimali za maji zinalindwa na
kuendelezwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na baadaye.
Yapo mambo makubwa yaliyofanywa na Wizara ya Maji kupitia idara hii ili kuhakikisha Mtanzania anaendelea kunufaika na rasilimali hii muhimu ambayo tunaweza sema ni Zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni jukumu la kila mtu kuwa na wivu nayo. Mpaka sasa jumla ya vyanzo vya maji 59 vimetangazwa katika Gazeti la Serikali kuwa maeneo tengefu ya maji. Eneo la ufuatiliaji wa mwenendo wa maji nchini hufanyika kupitia vituo maalum ambapo mpaka sasa kuna idadi ya jumla ya vituo 1,265.
Uchafuzi,
uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji unaotokana na kuongezeka kwa shughuli
za kiuchumi na kijamii huchangia kwa sehemu kubwa kupungua na kuzorota kwa
ubora wa rasilimali za maji na huathiri uendelevu wa rasilimali za maji nchini.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo Serikali
kwa kushirikiana na wadau, imeendeleza uhifadhi na udhibiti wa uchafuzi wa
vyanzo vya maji kupitia mipango mbalimbali inayojumuisha kutoa elimu kwa jamii
juu ya umuhimu wa kutunza na kulinda vyanzo vya maji; pamoja na kutambua,
kuweka mipaka, kutangaza kwenye Gazeti la Serikali na kurejesha vyanzo vya maji
vilivyoharibika
Ili kujali afya ya watumiaji wa maji,
serikali ya awamu ya sita imehakikisha inaendeleza matumizi ya majisafi na salama
kwa kuimarisha maabara za ubora wa maji ambapo hadi sasa Wizara ya Maji inazo
maaara za ubora wa maji 17 ambazo ziko sehemu mbalimbali mikoani. Maabara Saba kati
ya hizo zina ithibati ya kimataifa, zinaweza kufanya kazi katika kona yoyote ya
dunia hii. Mipango inayoendelea ni kuhakikisha maabara zote zinakuwa na vyeti
vya ithibati ambavyo vitazifanya kutambulika kimataifa.
Eneo lingine ni utekelezaji wa kazi, miradi na programu mbalimbali ambazo hufanyika kupitia Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Maji. Mpaka sasa Wizara ya Maji inazo Mamlaka za Maji 89, Wakala za Serikali tatu, Vyombo vya Utoaji Huduma Ngazi ya Jamii (CBWSOs) 1,946 na Bodi za Maji za Mabonde tisa.
Athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo ukame wa muda mrefu, kuchelewa kwa mvua pamoja na mafuriko pia zimeendelea kuathiri Sekta ya Maji katika nchi mbalimbali, kwa kuchangia kukauka kwa vyanzo vya maji, kuongezeka kwa migawo ya maji pamoja na kuharibika kwa miundombinu ya maji.
Hapa nchini, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inaendelea kuhimiza ushiriki wa wananchi katika utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na mazingira. Vilevile, Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kutekeleza miradi ya maji ambayo itatumia vyanzo vya maji vya uhakika kama vile mito mikubwa na maziwa na ujenzi wa mabwawa ya kuvuna maji ya mvua.
Kwa hakika uongozi wa Rais Samia
katika Sekta ya Maji unaacha alama chanya ambazo hazitafutika katika vinywa na
Maisha ya watanzania.
0717697205


Comments
Post a Comment