Hati fungani ya kwanza ya miundombinu ya maji kusini mwa jangwa la Sahara yaingia soko la Hisa la Dar
Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) akipiga kengele kuashiria Hati fungani ya Tanga UWASA kuingia rasmi katika soko la hisa la Dar es Salaam
Hati Fungani ya Kijani ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) hatimaye imeingia sokoni rasmi katika soko la hisa la Dar es salaam, na kuwa Taasisi ya kwanza ya umma inayotoa huduma katika jamii kuingia katika soko hilo.
Tanga UWASA inakuwa Mamlaka ya Maji ya kwanza katika taasisi za Umma kuingia katika soko la Hisa kwa nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano na darasa kwa nchi nyingine.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) ambaye pia ni mtaalamu wa masoko ya hisa ameongoza kazi hiyo kwa niaba ya Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba(Mb) jijini Dodoma.
Mhe. Bashungwa ameishukuru Wizara ya Maji na serikali kwa ujumla kwa kuingia katika utaratibu huo na kuzitaka taasisi nyingine za serikali kuiga mfano huo na kusema itasaidia serikali kusonga mbele kwa kupata chanzo mbadala cha fedha badala ya kutegemea bajeti ya serikali.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ambaye amehudhuria hafla hiyo amewapongeza Tanga UWASA kwa kutafsiri maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha akina mama wote nchini wanapunguziwa majukumu kwa kufikishiwa huduma ya maji katika maeneo yao “kumtua mama ndoo yam aji kichwani”.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji Tanga UWSSA Mhandisi Geofrey Hill amesema malengo ya awali ilikuwa kukusanya shilinigi Bilioni 53.1 ambapo kiasi kilichokusanywa kilifika shilingi Bilioni 54.72.
Amesema fedha hizo zitasaidia kupanua miundombinu ya maji ikiwemo ujenzi wa tenki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 35 . Aidha, upanuzi huo utawezesha maji kupatikana kwa asilimia 100 Tanga mjini wakati huduma ya maji katika miji mingine inayohudumiwa na Tanga UWASSA itafikia asilimia 95 badala ya asilimia 70 zinazotolewa sasa.
Mhandisi Geofrey Hill
Eneo jingine litakaloboreshwa kwa wananchi ni utoaji wa huduma ya Dira za maji za malipo kabla ambapo Dira 10,000 zitanunuliwa. Pia, uzalishaji maji utaongezeka kutoka lita za ujazo elfu 45 hadi lita elfu 60 na kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 30 hadi 20.. Uzinduzi wa Hati fungani ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga ulifanyika jijini Tanga Februali 22, 2024 ukiongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.

.jpg)



Comments
Post a Comment