Miaka 50 ya Chuo cha Maji na simulizi ya ‘Endala Kubhi.’
Tarehe 31 Januari, 2024 Chuo cha Maji kilifikisha miaka 50 tangu kianze kuandaa watalaam wa Sekta ya Maji hapa nchini. Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alijionea tukio hili katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
VIDEO YA MIAKA 50 YA CHUO CHA MAJI BOFYA HAPA
Washiriki wengine walioshuhudia tukio hilo ni pamoja na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), washirika wa maendeleo na wadau wengine wa sekta ya maji ambao walikuwa wajumbe na wakishiriki Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kisayansi la Maji linaloandaliwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Chuo cha Maji.
Mengi yaliyozungumzwa katika tukio hilo na yaliamsha simulizi
nyingi za kusisimua kuhusu mipango na mkakati wa kuiwezesha serikali ya
Tanzania kuwa na wataalam wabobezi katika fani ya maji. Yapo yaliyozungumzwa na
Mgeni Rasmi Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kiwete. Yapo yaliyozungumzwa kupitia video
fupi ambayo ilikusanya ushuhuda wa waliowahi kuwa viongozi wa taasisi hiyo muhimu
na wasomi waliopata utaalam wao katika Chuo cha Maji.
Pia, viongozi wa sasa wa Sekta ya Maji akiwemo Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb). Ni hakika muendelezo wa tukio kuanzia mwanzo hadi mwisho wake wahusika wote walistahili ‘maua yao’ kuhusu masuala ya maji. Waliandaa tukio likapendeza, likafana, likaionesha seka ya maji ilivyopiga hatua nchini Tanzania, kwa historia hadi hivi sasa.
Simulizi zilidhihirisha mikakati bora inayofanywa na viongozi waliopita na waliopo sasa kuanzia kwa waziri mwenye dhamana Mhe. Jumaa Aweso (Mb) kuhakikisha chuo hicho kinajipambanua kuwa tanuru la kupika na kuzalisha wasomi wenye fikra tunduizi ndani ya malengo ya awali ya kuanzishwa kwake kuhusu huduma ya maji kwa jamii.
Simulizi zilieleza jinsi waliotangulia kuongoza serikali walivyoonesha nia ya dhati ya kuhakikisha fursa ya hicho chuo kunufaisha nchi ya Tanzania kwanza, badala ya nchi nyingine za Afrika ambazo pia zilikuwa katika kinyanganyiro hasa baada ya azimio kutoka katika vikao vya iliyokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU). OAU iliazimia kujengwa chuo cha kuandaa wataalam wa maji Afrika bila kuainisha wapi na eneo la kujenga.
Mapambano haya ya kuivutia fursa nchini Tanzania ndiyo yanayokumbusha simulizi ya Endala kubhi maarufu kwa Wakerewe ambayo kwa Kiswahili inafanana kwa karibu sana na msemo wa Kiswahili unaotumika usemao ‘Anayelala na mgonjwa ndiye anayejua mihemo yake.’
Kisa cha ‘Endala Kubhi’ kutoka kwa Wahenga wa Kikerewe kinaanzia kipindi ambacho kisiwa cha Ukerewe kilikumbwa na upungufu wa chakula. Hali hiyo ya uhaba ilienda sambamba na upepo mkali ambao ulikuwa ukivuruga hali ya ziwa Victoria na kufanya kazi ya uvuvi kuwa ngumu tofauti na wenyeji walivyozoea.
Katika mazingira hayo magumu ya kupata chakula mzee mmoja mzoefu wa kazi ya uvuvi aliendelea kupambana na huo upepo mkali maarufu kisiwani hapo kama ‘Omlimbe’. Mwisho wa siku Mzee huyu alikuwa akirudi na samaki wa kutosha kwa familia yake na majirani wachache waliomzunguka.
Alipokuwa akiulizwa na wenzake kwa nini anahatarisha maisha yake kiasi hicho, jibu lake lilikuwa ni fupi sana. Endala kubhi niyo ekwimanya. (aliyelala vibaya/aliyelala na njaa ndiye anajijua). Msemo huo ukazaa methali ya Kikerewe, ‘Endala kubhi niyo ekwimanya.’ Waswahili wakasema anayelala na mgonjwa ndiye anajua mihemo yake.
Dkt. Adam Karia ni Mkuu wa Chuo hicho (Rector). Anatoa
pongezi kwa viongozi wote waliotangulia kwa kuona umuhimu wa kuwa na chuo
ambacho kinazalisha wasomi ambao wataweza kusaidia maendeleo ya Sekta ya Maji,
hapa nchini na nje ya nchi pia.
Heshima za kipekee anazielekeza kwa uongozi wa awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wake wa Maji Mhe. Aweso. Anasema yeye kama Mkuu wa Chuo amekuwa na nafasi ya kufanya makubwa yanayoonekana leo hii kutokana na utayari wa viongozi hao walio juu yake kuanzia kwa waziri mwenye dhamana ya chuo hicho Mhe. Jumaa Aweso (Mb) hadi Rais wa Tanzania Mhe .Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Anasema ndani ya kipindi chake cha uongozi amekuwa na mazungumzo na Waziri Aweso ambaye pia amekuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha chuo hicho kinapewa fursa zote za kukiwezesha kifanye kazi. Jitihada hizo zimewezesha maboresho makubwa kuonekana katika kipindi cha awamu ya sita. Chuo hicho hivi sasa kina miundombinu ambayo inaonekana wazi na inayowezesha mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia.
“Nimekuwa Mkuu wa Chuo tangu Januari 2020. Sasa natimiza
miaka minne. Kuanzia mwaka huo tumeendeleza kazi ambayo wakuu wengine walikuwa
wanaifanya lakini sisi tumeifanya kwa staili tofauti. Tumefanya maboresho makubwa
kutokana na utayari wa viongozi wetu wa serikali ya awamu ya sita. …tumejenga maktaba
kubwa. Naamini katika vyuo vya elimu ya juu nchini pengine inaweza kuwa maktaba
ya pili kwa ukubwa.” Dkt. Karia anasema na kufafanua kwamba Maktaba hiyo
inaweza kuhudumia zaidi ya wateja wa kusoma 600 kwa wakati mmoja.
Anasema Chuo kimejenga madarasa mapya 17. Kimekarabati mabweni sita likiwemo bweni ambalo limepewa jina la Mhe. Aweso kama kumbukumbu kwa makubwa aliyotekeleza katika chuo hicho. Anasema yote hayo yamewezekana kutokana na utayari wa viongozi walioko madarakani hapa nchini.
Mkuu wa Chuo hicho kwa kipindi cha awamu ya tatu Mhaidrolojia Washing’ton Nyakale
Mtayoba ambaye amekiongoza chuo hicho kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 1992 amesimulia
historia kwamba uamuzi wa kujenga Chuo cha Maji uliibuliwa katika vikao vya taasisi
ya nchi za Afrika yaani Umoja wa Nchi huru za Kiafrika (OAU) kupitia Tume yake
ya Uchumi (Economic Commission for Africa).
Anasema kwamba uamuzi huo haukuwa kwamba chuo kijengwe nchini Tanzania bali iliamuliwa ndani ya kikao kijengwe chuo mahali fulani Barani Afrika ili kisaidie mahitaji makubwa ya wataalam wa sekta ya maji na kusaidia shughuli nyingine zinazotokana na maji.
Anasema wakati huo pia serikali ya Tanzania ilikuwa ikiendesha Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa hiyo ilikuwa ni fursa muhimu ya kuchangamkia kwa sababu wao ndio walikuwa wakilala na mgonjwa. Wao ndio walikuwa wakijua mahitaji ya Taifa kama mzee Endala Kubhi wa Ukerewe alivyokuwa akijua mahitaji ya familia yake. Wakafanya kila jitihada kushawishi ili chuo hicho kijengwe nchini Tanzania, hilo likafanikiwa.
Hivyo, Chuo kikaja Tanzania chini ya Mkuu wake wa kwanza raia wa nchini Sweden Bwana Carl Eric Westberg mwaka 1974 wakati huo kikiitwa Water Resources Institute, baadaye kikaitwa Rwegarulila Water Institute ikiwa pia ni kumbukumbu ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, mwaka 1974, Wizara ambayo ndiyo iliyokuwa na dhamana ya maji wakati chuo kinaanzishwa. Baadaye kikaitwa Water Development and Management Institute. Hiyo ni historia, na leo hii chuo kinaitwa Water Institute (Chuo cha Maji)
Ndoto ya Mkuu wa Chuo hicho kwa sasa Dkt. Karia ni kukiweka kuwa Chuo cha Maji Kikuu na cha Kimataifa ambacho kinaweza kupambana na vyuo vikuu vya mataifa mbalimbali duniani vilivyojikita katika masuala ya maji.
Mheshimiwa Kikwete anaziona ndoto za Dkt Karia zinatimia sasa
kwa uwekezaji mkubwa wa Serikali. Anampongeza kwamba amefanya mageuzi makubwa
ikiwemo kuwa na mtaala ambao unasaidia kupata ajira kwa haraka na kujiajiri.
(Competence Based) Anasisitiza kuwa wasomi waliozalishwa na chuo hiki wamekuwa
ni msaada mkubwa katika kulisogeza mbele taifa katika Sekta ya Maji. Uhalisia
unabaki kuwa maji ni huduma muhimu katika jamii ya Watanzania, hivyo chuo
kinachoandaa wataalam wa maji nacho ni lulu kwa jamii.

Comments
Post a Comment