Kigoma na mkakati wa kumaliza changamoto ya huduma ya majisafi
Ndoto na malengo ya viongozi waliopewa dhamana ya kutoa huduma ya maji mkoani Kigoma ni kuhakikisha huduma hiyo inamfikia kila mwananchi Mkoani hapo katika muda uliopangwa.
Hilo ni jukumu la msingi ambalo limewafanya watendaji hao waendelee
kuaminika mkoani hapo kwa wanavyopambana kuhakikisha malengo ya serikali
yanatimia. Wanasema wanachi wa mkoa huo wakiwemo akina mama wanajituma sana
katika shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo kazi za kilimo na biashara. Hivyo,
kuwafikishia huduma ya majisafi na salama katika makazi yao kutapunguza eneo
moja la kutumia muda mrefu katika maji na kubaki na shughuli na fursa nyingine
tele zilizowekwa na serikali za kuongeza kipato.
Eneo la makao makuu ya mkoa huu linahudumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA). Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA Poas Kilangi anaishukuru serikali kwa kukamilisha mradi wa Kuboresha Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Kigoma ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya maji katika mji huo, ambapo ziwa Tanganyika ndio chanzo cha maji yaliyochokuliwa eneo la fukwe ya Amani, Kata ya Bangwe.
Kwa upande wa Vijijini huduma ya majisafi inatolewa na Wakala
wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ikiongozwa na Meneja wa Mkoa Mhandisi Mathias Mwenda.
Mhandisi Mwenda anasema ushuhuda wa mafanikio ya huduma ya
maji katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Kigoma ziko wazi kwa macho ya kila
binadamu kwani miradi inaonekana kila kona. Pia ushuhuda uko wazi katika vinywa
vya wanufaika kutokana na adha waliyokuwa wakiipata kabla ya kuwezesha huduma
hiyo kuwafikia walengwa.
Anakiri kwamba bado kuna changamoto sehemu tofauti tofauti
lakini jitihada ziko wazi katika kuhakikisha ndani ya kipindi kilichopangwa
huduma hiyo inawafikia wananchi wote. Mhandisi Mwenda akiongea hayo anawaahidi
wananchi wa Kigoma wasiwe na shaka au wasiwasi kwasababu serikali inatambua
changamoto hiyo na iko mbioni kuitatua kwa kuwaletea faraja.
Anasema eneo analohudumia kuna jumla ya vijiji 306, ambapo vijiji
231 vimeshapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza. Vijiji 30 vina
huduma ya maji ambayo bado inafanyiwa kazi ili iwe imara zaidi, wakati vijiji
33 vipo mbioni kupatiwa huduma. Anasema matajarajio ni huduma hiyo kuwafikia
wananchi wa vijiji vyote kwa haraka.
Mhandisi Mwenda anarejea
kumbukumbu inayompa matumaini kwamba RUWASA ilianzishwa mwaka 2019 wakati huo
huduma ya majisafi na salama mkoani hapo ilikuwa ni asilimia 61. Pamoja na
hilo, katika miaka minne ya utekelezaji wa kazi, huduma hiyo imepanda hadi
kufikia asilimia 70.8 Anafafanua kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji
wa idadi ya miradi 136. Malengo ni kuhakikisha huduma hiyo inasambazwa kwa kila
mwananchi wa mkoa wa Kigoma na kwamba uwekezaji unaofanywa na serikali ni mkubwa.
Mhandisi Mwenda anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utayari wake wa kuhakikisha huduma ya majisafi
na salama inafanikiwa kila sehemu mkoani hapo. Aidha, anamshukuru Waziri wa
Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) na timu nzima ya Wizara ya Maji kwa kuwa tayari
kuhakikisha ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa mipango hiyo unakwenda
vizuri
Anatolea mfano wilaya ya Buhigwe ambayo anakiri ilikuwa moja
ya wilaya ambazo zilikuwa na changamoto wakati RUWASA inaanzishwa lakini sasa
matumaini ya wananchi yamekuwa makubwa zaidi.
Wilaya hiyo ina jumla ya vijiji 44 ambapo vijiji 30 vina
huduma ya majisafi na salama, vijiji 10
vina huduma ya majisafi lakini bado inahitaji kuimarishwa wakati vijiji vinne vipo
katika mkakati wa kufikishiwa huduma.
Kwa ujumla huduma ya majisafi katika wilaya hiyo imefikia
asilimia 70.2. na vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma vikiwa na matumaini makubwa
ya kufikiwa kwa muda mfupi.
Vijiji nane kati ya 10 vyenye huduma ambayo haitoshelezi vipo kwenye mpango na miradi yake ipo katika hatua za utekelezaji kwa ajili ya kupelekewa huduma ya mtandao wa mabomba ya maji, vijiji viwili kati ya vinne ambavyo havina huduma ya maji kabisa vipo katika mpango wa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kuanza kujenga miundombinu ya maji ya bomba. Mipango ni kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na huduma ya majisafi na salama kwa haraka.
Kijijini Migongo katika wilaya ya Buhigwe. John Fransis Mollel ambaye ni Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Buhigwe, anasema kijiji hicho ni moja ya vijiji vilivyokuwa na changamoto kubwa ya maji, na utekelezaji wa mradi wa maji wa Migongo umewezesha eneo hilo kupata huduma ya maji kwa wananchi wote.Mradi
mwingine ambao unatarajiwa kuwa mkombozi katika wilaya hiyo ni mradi wa maji wa
Munanila-Nyakimue utakaohudumia vijiji nane ukitajwa ukiwa na thamani ya
shilingi bilioni 8.2
Meneja Mollel anasema mradi huo utawezesha huduma ya majisafi
kufika asilimia 85 na hivyo kufikia lengo la Serikali la huduma ya maji
vijijini kufika asilimia 85 ifikapo mwaka 2025. Anasema nia hasa ni kuhakikisha
huduma ya majisafi wilayani Buhigwe inakuwa zaidi ya asilimia 85, pia kuhakikisha
akina mama wa Buhigwe wanasahau adha ya huduma ya majisafi, na salama, kwa
kufanya kazi nyingine za maendeleo.
Maelezo ya Meneja Mollel yanapata uthibitisho kutoka kwa familia za wanufaika ikiwemo familia ya mzee Bosco Sunzu Njinyari wa Kijiji cha Migongo. Mzee Njinyari anaishukuru serikali kwa kutekeleza mradi wa maji wa Migongo. Anasema mradi huo umembadilisha kiuchumi kwani umemuwezesha kuimarisha shughuli ya ufugaji ikiwamo wa kuku, bata na mbuzi mifugo ambayo inamuingizia kipato. Pia amekuwa mkulima mzuri kwani anaotesha miche ya bustani katika makazi yake karibu na eneo la Bomba. Miche hiyo inahamishwa kupelekwa mashambani na hatimaye kuongeza mapato ya kilimo.
Wanufaika wengine wa huduma ya majisafi katika Kijiji hiki ni
Emakulata Deodatus. Anasema amejikomboa kwa kiasi kikubwa baada ya kupata
huduma ya maji. Anasema usumbufu ulikuwa mkubwa kutokana na asili ya eneo hilo
lenye miinuko na mabonde. Emakulata anaongeza kuwa sasa hali ni nzuri, usafi
umeongezeka, usumbufu umeisha.
Mwingine ni Dules Manase ambaye anashuhuda ya adha ya kuamka
saa 12 kwenda mabondeni kutafuta huduma ya maji. Anakiri kwamba maji hayana
mbadala hivyo kinachoendelea sasa ni shukrani kwa serikali inayoongozwa na Rais
Samia suluhu Hassan. Hawakuwa na uwezo wa kutunza bustani kipindi cha kiangazi
lakini sasa inawezekana.
Mkazi mwingine Bi. Veronica Chuma anasema huduma ya maji hayo yamempunguzia adha ya kuchota maji kutokana na umri wake mkubwa. Anasema kuna nyakati hasa kiangazi mabwawa yalikuwa yanakauka maji hivyo maisha yanakuwa ya kubahatisha kwani kunakuwa hakuna maji.
Bi. Chuma anasema bei za maji vijijini ziangaliwe ili huduma
hiyo iwe endelevu na kuwapa fursa wananachi kufanya kazi zaidi.





.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
Comments
Post a Comment