Huduma ya majisafi ilivyopunguza zaidi ya asilimia 50 ya magonjwa ya kuhara.
Julai 24, 2022 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alizindua mradi wa maji wa Sibwesa wilayani Tanganyika mkoani Katavi. Mradi huo unahudumia zaidi ya wakazi wapatao elfu nane wa kata ya Sibwesa. Katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) alimwakilisha Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb).
Baadhi ya maelekezo na maagizo
aliyoyatoa Makamu wa Rais ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha mradi huo unakuwa
msaada wa kupunguza adha ya changamoto ya huduma ya majisafi na salama kwa
wananchi ikiwemo kuwaepusha na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na matumizi
ya maji yasiyo salama.
Ikiwa ni takribani miezi 18
tangu mradi huo uzinduliwe, mradi umeleta mabadiliko makubwa katika eneo la
afya ya jamii. Dkt. Miriam Lulandala ni Mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Sibwesa
ambacho kinahudumia wananchi wengi ambao wananufaika na huduma ya maji kutoka
mradi huo.
Anasema baada ya Serikali kusambaza
mabomba ya huduma ya maji kutoka katika mradi wa maji Sibwesa magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo
salama yamepungua kutoka wastani wa wagonjwa 80 kwa mwezi kwa mwaka 2020 wakati
ambao mradi huo ulikuwa haujaanza kutoa huduma hadi kufikia wagonjwa 34 kwa
mwezi kwa mwaka 2023 ambapo mradi umesambazwa na kufikishwa katika makazi ya wananchi
wengi.
Mradi huo ulianza kutoa huduma
mapema mwezi Aprili 2021 mwaka ambao matatizo yanayotokana na magonjwa ya hayo
yaliyoelezwa na mtaalamu wa afya ya binadamu yalianza kupungua.
Dkt. Miriam anasema mwaka 2020
kuanzia Julai hadi Desemba kituo hicho kilipata wagonjwa wa magonjwa ya yanayosabishwa
na kunywa maji yasiyo salama inayofikia 477 ambayo ni sawa na asilimia 79.5 kwa
mwezi. Mwaka 2021 mradi ulipoanza kutoa huduma wagonjwa wa aina hiyo kwa miezi
hiyo sita walipungua na kufikia 373 sawa na asilimia 62.1 wakati mwaka 2022
mradi ulipoendelea kupanuliwa na kuwafikia wananchi wengi, kituo hicho
kilipokea wagonjwa 274 sawa na asilimia 46.
Baada ya miundombinu ya mradi
huo kusambazwa na kuwafikia wakazi wengi zaidi, hali imebadilika kwa kiasi
kikubwa. Anasema mwaka 2023 kuanzia mwezi Julai hadi Desemba takwimu za afya za
kituo kituo zinaonyesha wagonjwa wa aina hiyo waliopokelewa na kuhudumiwa ni 203 tu, ambayo ni sawa na wastani wa wagonjwa
34 kila mwezi.
“Hili ni suala la kumshukuru la kumshukuru
Mungu kwa huduma yam aji kwa wananchi. Ni sadaka kubwa ambayo serikali imeamua
kuwapa wananchi wa Sibwesa ili kulinda afya zao”. DKt. Miriam anasema huku akiiomba
serikali iendelee na jitihada hizi ili kuhakikisha maeneo yote nchini
yanafikiwa na huduma ya majisafi na salama ili kulinda afya za wananchi.
Anasema kabla ya kupata huduma
hii wananchi walikuwa wakitumia maji kutoka madimbwi na visima vya kienyeji
ambavyo walikuwa wakitumia pamoja na mifugo hali ambayo ilikuwa ikisababisha
kupata maradhi ya mbalimbali yasababishwayo na matumizi yam aji yasiyokuwa
salama.
Anasema changamoto nyingine
iliyokuwa ikisababisha ongezeko la magonjwa, ni kwa akina mama waliokuwa wakienda
kituoni kupata huduma ya kujifungua
walikuwa wakilazimika kuondoka na nguo zao chafu kwenda kufanyia usafi nyumbani
hali ambayo ilikuwa ikisababisha maambukizi mapya ya magonjwa katika makazi
yao.
“Si huduma ya maji ya usafi
tu, sasa hivi hata huduma ya maji ya kunywa kwa watoto na wazazi ipo na maji
hayo ni safi na salama hivyo afya imeendelea kuimarika kwa kiasi cha kutosha
katika maeneo yanayonufaika na mradi huu.” Dkt. Miriam anasema
Ushuhuda huu wa Dkt. Miriam
unaungwa mkono na Shamira Kiwele mkazi wa
Sibwesa. Shamira anasema ni Mama wa Watoto wawili ambaye mtoto wake wa
pili alijifungilia hapo kituoni katika kipindi ambacho hakukuwa na huduma ya
majisafi na salama.
Anakumbuka yaliyotokea akisema
ndugu zake waliomsindikiza kumuuguza ilibidi wahangaike kupata maji ya kwa
ajili ya usafi. Anashukuru kwamba pamoja na usumbufu huo wa huduma ya majisafi
na salama, wahudumu wa afya katika kituo hicho walikuwa wakipambana sana
kuhakikisha mzazi anaendelea kuwa salama wakati wote.
Shamira Kiwele, mkazi wa Sibwesa.
Anashukuru huduma hiyo kuingia katika maeneo
hayo ikiwepo majumbani kwani licha ya kupata huduma ya majisafi na salama kwa
wazazi shughuli za kiuchumi na kijamii zimeimarika. Ratiba ya kazi za kifamilia
imekaa vizuri kwani ratiba muhimu ya kusafiri umbali mrefu kutafuta maji
imeisha.
Diwani wa kata hiyo Mhe. Deusi
Masunga anasema sasa malalamiko aliyokuwa akikutana nayo kutoka kwa wananchi
yamekwisha. Anaiomba serikali iendelee kuwekeza katika huduma za kijamii na
anatoa shukrani kwa Wizara ya Maji kwa kuhakikisha huduma hiyo ya majisafi na
salama inafika katika vituo vyote vya huduma za kijamii katika kata yake.
Anasema maji hayo yamewezesha
kuanza ujenzi ili kupanua kituo hicho cha Afya cha Sibwesa kwa sababu
changamoto ya huduma ya maji ya ujenzi haipo tena.
Meneja wa Wakala wa Maji na
Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Tanganyika Mhandisi Alkam Sabuni
anasema wanatambua umuhimu wa huduma ya
majisafi kwa jamii hasa katika suala la afya. Kwa kutambua hilo walihakikisha
wanafikisha huduma ya majisafi katika vijiji vyote vilivyoko katika kata hiyo
si kwa wananchi tu bali wamehakikisha maji hayo yafikishwa katika vituo vyote
vya huduma za kijamii.
“Kata hii ya Sibwesa inazo
Taasisi za Umma sita na zote tumezifikishia huduma ya majisafi na salama” Sabuni anasema na kusisitiza kuwa wameaminiwa
kufanya kazi, hivyo ni lazima watimize wajibu wao.
“Tumeapa na tumeaminiwa
kuhakikisha tunafikisha huduma kwa wananchi. Hilo ndilo tunalolizingatia na
tunashukuru Serikali yetu pamoja na uongozi wa ngazi ya juu ya wizara na RUWASA
makao makuu wanatuunga mkono.” Anasema Alkam Sabuni.
Anasema Wilaya ya Tanganyika anayoihudumia ina vijiji 55
vyenye wakazi wapatao 375,000. Vijiji takribani 39 vyenye wakazi wapatao
330,000 vimefikiwa na huduma ya majisafi na salama na hivyo kufanya asilimia ya
wananchi wanaopata huduma hiyo kufikia 81.
Anasema kwa aina ya miradi
inayoendelea kutekelezwa kwa fedha ya Serikali katika wilaya hiyo matumaini ni
kuwa mwaka wa fedha 2024/2025 huduma ya majisafi na salama itafikia asilimia
92. Jambo walilozingatia, ni kwa Taasisi zote za umma katika vijiji vyote 39
walivyovifikia wamepelekewa huduma ya majisafi na salama hali ambayo imewezesha
usalama wa kiafya kwa watu wengi wa wilaya ya Tanganyika.
0717697205


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)


Comments
Post a Comment