Hongera sekta ya maji kuwa namba moja Duniani 2023.
Na Evaristy Masuha.
Zawadi hizi
zinazotolewa kutokana na idadi ya magoli yaliyopatikana katika mechi husika za
kimataia. Hili limekuwa likifanyika kwenye mechi za kimataifa ambapo wanufaika
wakuu wamekuwa ni timu ya Taifa ya Tanzania pamoja na timu kongwe za Simba na Yanga
ambazo hadi sasa zinashiriki mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika.
Wakati Rais Samia akiwapima na kuzizawadia timu zake za hapa
nchini, upande wa Sekta ya Maji Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ambayo inaongozwa na Mhe. Rais Samia inapimwa na kupambanishwa na mataifa
mbalimbali katika kunufaika na fedha zinazotolewa na Benki ya Dunia.
Fedha hizo zinavunwa kupitia Progam ya Endelevu ya Usambazaji
Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (SRWSSP) ambapo wanufaika wa eneo hili
wanalipwa kutokana na matokeo ya mradi uliotekelezwa. Mpango huu maarufu kwa
jina la Lipa kwa Matokeo (PforR).
Kupitia PforR, Benki ya Dunia hutoa fedha na kufanya ufuatiliaji.
Uwezekano wa kuongezewa fedha zaidi unatokana na idadi ya watu ambao nchi
husika imeweza kuwafikishia huduma ya majisafi wananchi wake. Idadi kubwa ya
watu uliowafikishia huduma vinaamua kiwango cha fedha unachostahili kupata ili
kuendelea kuwafikia wanufaika zaidi.
Kwa vile mavuno ya fedha husika yanatokana na huduma katika Sekta
ya Maji ni wazi msimamizi mkuu wa eneo hili, aliyeaminiwa na Rais Samia ni
Waziri wa Maji. Ingekuwa kwenye soka huyu ndiye Kocha Mkuu aliyeamiwa na timu
husika kukamilisha mipango na ushindi. Hivyo, Waziri wa Maji anafanikisha
hitaji la bosi wake Rais Samia kuhakikisha anakimbizana na utekelezaji wa
miradi bora ya maji ili kuvuna zaidi fedha hizi na kupunguza machungu ya huduma
ya majisafi kwa wananchi.
Ifahamike kuwa licha ya idadi ya watu uliowafikishia mradi,
Benki ya Dunia inachukua hatua kujiridhisha kuhusu ubora wa mradi na uendelevu
wake.
Waziri Aweso anafahamika kama shabiki wa mpira wa miguu,
pamoja na michezo mingine pia na mara kadhaa amekuwa akitania watendaji wake
kwamba katika kuhakikisha huduma ya maji inamfikia kila Mtanzania yeye
anasimama kama Benchika, Kocha Mkuu wa Simba.
Nianze kwa kumpongeza huyu Benchika wa Sekta ya Maji kwa
kufunga mwaka bila kumuangusha Bosi na wadau wake. Mhe. Aweso anafunga mwaka
akitembea kifua mbele kwa kuwa namba moja kati ya zaidi ya mataifa 50
yanayoshindana katika kuvuna fedha za PforR.
Taarifa ya kuwa bingwa katika eneo hili ilitajwa na Makamu wa
Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Victoria
Kwakwa katika mkutano uliohusu Maji na Usafi wa Mazingira (Wash Leadership
Summit) uliofanyika Novemba 14-15, 2023, Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Mkutano huu ambao ulikuwa ukijadili masuala mbalimbali
ikiwemo utekelezaji wa mradi huo uliwahusisha mataifa mbalimbali yanayotekeleza
program hii, Tanzania ikatajwa kuwa kinara wa utekelezaji wa miradi hii. Kwakwa
alienda mbali kwa kuwataka mataifa mengine yajifunze kutoka Tanzania.
Mafanikio haya hayajaifanya Dunia kukaa kimya. Hata kabla ya
tangazo hilo, Benki ya Dunia ilishachukua hatua ya kuyashauri mataifa
mbalimbali ambayo yanakutana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa
miradi hiyo kuja kujifunza Tanzania.
Miezi michache iliyopita timu ya wataalama kutoka nchini Nigeria
ilikuwepo hapa nchini kwa ajili ya kupata uzoefu wa miradi hii ya P4R. Wataalam
wa Sekta ya Maji kutoka Tanzania wamepata fursa ya kutembelea nchi mbalimbali
duniani kushirikishana uzoefu na mafanikio. Hongereni tena wizara ya maji kwa
kuendelea kuitangaza Tanzania na kuonesha kwamba Tanzania inaweza.
Ndani ya miaka mitatu, Benki ya Dunia iliridhishwa na kasi ya
utekelezaji wa miradi kupitia mpango huo ambapo Tanzania ilikuwa imefikisha
maji kwa zaidi ya watu wapya milioni 4.7 kwa mikoa 17. Licha ya kufikisha
huduma ya majisafi kwa wanufaika Benki ya dunia ilijiridhisha kwamba miradi
iliyotekelezwa kupitia mpango huo ilikuwa na ubora unaostahili katika viwango
vya kimataifa.
Kutokana na matokeo hayo Benki ya Dunia imeiongeza Tanzania Dola
za Marekani milioni 300. Licha ya hivyo,
imeiruhusu Tanzania kupanua wigo wa utekelezaji wa miradi kutoka mikoa
17 hadi kufikia mikoa 25.
Mafanikio haya yanaongeza kasi ya kufikia malengo
yaliyoainishwa na Serikali kufikia mwaka 2025 huduma ya maji vijijini iwe
imefikia asilimia 85 wakati mijini huduma hiyo ikiwa imefikia asilimia 95.
Taarifa za Wizara husika ya Maji zinaonesha kwamba hadi
wizara inafunga mwaka huduma ya maji mijini na vijijini imefikia wastani wa
asilimia 81 ambapo kwa mjini ni wastani wa asilimia 88 na vijijini ni wastani
wa asilimia 77. Vijiji vilivyo na huduma ya maji ni 9,259 kati ya vijiji
12,318.
Aidha, jumla ya miradi 506 ilikamilishwa ikiwemo 436 ya
vijijini na 70 ya mijini yenye uwezo wa kuhudumia wananchi 5,754,340 (3,145,645
wa vijijini na 2,608,695 wa mijini).
Mheshimiwa Aweso anawapa
matumaini Watanzania na Dunia kwa ujumla kwamba taratibu zinaenda vizuri kwani
miradi iliyopo ni mingi na itawezekana huduma hiyo kupanda kwa kiwango kikubwa.
Aidha hakuna mashaka kuwa malengo ya serikali yatafikiwa na hata kuzidi.
Kila raheli Sekta ya Maji.
kila la heri wadau wa maji. kila la heri Watanzania katika 2024.


.jpeg)







Comments
Post a Comment