Aweso na ile ndoto ya 2020. Ni suala la Muda tu, Tabora watashuhudia.
Shughuli ya Uchimbaji wa Mtaro na usambazaji wa mabomba
mradi wa maji wa Miji 28 unaendelea katika pori la Maswanya wilayani Uyui,
Mkoani TaboraNa, Evaristy Masuha
Mwishoni mwa mwezi Julai 2020 nilibahatika
kufanya mazungumzo na Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso (Mb) wakati huo akiwa Naibu
Waziri wa Maji, kwa cheo chake cha kazi, na uwaziri wake hata haukumfanya awe
mbali kwamba ashindwe kujichanganya na kuongea mawili matatu, katika jamii yetu
hii ambayo kila kukicha mengi yanajiri.
Swali langu lilikuwa kutaka kujua hatma ya huduma ya maji katika wilaya zote za mkoa wa Tabora hasa baada ya
huduma hiyo kufikishwa katika miji ya Igunga, Nzega na Manispaa ya Tabora. Takribani miaka mitatu sasa tangu mazungumzo yale
yafanyike nimepata tena fursa ya kutembelea mkoa wa Tabora. Lengo likiwa lile
lile tulilochati na Mhe. Aweso, kuthibitisha iwapo ndoto yake imetimia.
Safari yangu imeanzia ofisini kwa
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) hadi
pori la Kijiji cha Maswanya kilichopo Uyui mkoani Tabora.
Mkurugenzi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) Mhandisi Mayunga Kashilimu akizungumza na mwandishi wa Makala hii katika eneo la pori la
Kijiji cha Maswanya, Wilayani Uyui Mkoani Tabora
Nakumbuka Mazungumzo yangu na
Mhe. Aweso ya mwaka huo wa 2020 yalitokana na mazungumzo yangu ya awali na
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa wakati huo Mhe. Aggrey Mwanri, naamini
bado twamkumbuka haswaa Mzee wa “Injinia soma hiyo”, pamoja na mazungumzo na baadhi
ya wananchi wa wilaya za mkoa wa Tabora ambazo hazikuwa na huduma ya majisafi
na salama.
Mazungumzo yangu na Mhe. Mwanri
ambaye bado anaendelea kukumbukwa kwa kuutangaza mkoa wa Tabora kama Toronto ya
Afrika yalifanyika juu ya tenki la maji
la Itumba lililoko mjini Tabora ukipenda “Tembo wa Tabora” akinionesha fahari
ya Tabora, Toronto ya Afrika. Akasema ujio wa maji ya ziwa Victoria na jitihada
za serikali zinazofanyika kuhakikisha maji haya yanasambazwa kila eneo la mkoa
huo linaileta Toronto ya kweli ambayo wengi walidhani ni masihara.
Alishukuru timu nzima ya Wizara ya Maji na serikali kwa ujumla
kwa kuhakikisha huduma hiyo ya majisafi na salama inamfikia kila mwananchi wa Tabora.
Sehemu ya mazungumzo yangu na Mheshimiwa Mwanri rejea yake inapatikanana katika
kiungo cha channel ya youtube, majiDigital anuani https://www.youtube.com/watch?v=nmnAzamKmDs&t=18s
Naibu Waziri Mhe. Aweso wakati huo, alinihakikishia kuwa hakuna mwananchi ambaye atapitwa na huduma ya majisafi na salama na kwamba watakaojaliwa kuwa hai ndani ya miaka mitano watashuhudia mageuzi na habari njema kabisa. Mhe. Aweso alirejea maneno yake ambayo amekuwa akiendelea kuyasema akinukuu kitabu cha Tenzi za Rohoni yasemayo ‘unapozuru wengine usinipite mwokozi’. Akasema Tabora ni njia ya kuelekea mkoa wa Mwanza ambako mradi wa maji wa ziwa Victoria unaanzia.
Waziri Aweso akiwa katika shughuli za ukaguzi wa miradi ya maji
“Sitathubutu kuwapita wananchi wa
Tabora na wilaya zake zote katika kuhakikisha maji ya ziwa Victoria yanawanufaisha”
alisema Mheshimiwa Aweso, akaenda mbali zaidi kwa kuahidi kuwa si wananchi wa
Mkoa wa Tabora tu bali wananchi wote wanaozungukwa na ziwa Victoria Mungu
akimjalia nguvu na afya na kuendelea kuaminiwa na mamlaka katika nafasi aliyoaminiwa
ndani ya Sekta ya Maji, atahakikisha huduma hiyo inamfikia kila mwananchi.
Sasa ni takribani miaka mitatu
tangu Mzee Mhe. Mwanri astaafu. Ni takribani miaka 3 tangu Waziri Aweso apewe
dhamana ya Uwaziri wa Maji. Nimepata fursa ya kutembela tena mkoa huu kwa lengo
hilohilo la kujifunza mabadiliko yaliyopo na hata kujihakikishia iwapo Toronto
ya Mwanri inaendelea. Iwapo wananchi wa mkoa wa Tabora hawajapitwa, nimekuwa
kama yule “Tomaso” ila sio kwa ubaya.
Fursa hii imeniwezesha kuzungumza
na viongozi wenye dhamana ya kuhakikisha majisafi, salama na yenye kutosheleza
yanafikishwa kwa wananchi. Mhandisi Mayunga Kashilimu ni Mkurugenzi Mtendaji wa
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora kwa kifupi ikijulikana kama
TUWASA.
Mhandisi Mayunga ananihakikishai
kuwa hadi kufikia Oktoba 2025 wilaya zote za mkoa wa Tabora zitakuwa zimefikiwa
na huduma hiyo. Anasema mkoa wa Tabora unajumla ya wilaya saba. Wilaya ambazo
hadi sasa zimefikiwa na huduma ya majisafi na salama kutoka ziwa Victoria ni
Igunga, Nzega, Tabora na Uyui.
Anaanza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa uthubutu wake wa kutenga
fedha ili kuwezesha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Tabora.
Anamshukuru Mheshimiwa Aweso kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha fedha hizo
zinafika kwa wakati na usimamizi unakuwa thabiti ili kuhakikisha tamani ya
fedha inaonekana kupitia utekelezaji wa miradi hiyo.
Anasema, kwa sasa mradi wa maji
wa miji 28 unaendelea kutekelezwa na kwamba mradi huo unasambaza mabomba yenye
urefu wa kilometa 190 ambazo zitawezesha miji yote ya makao makuu ya wilaya 3
ambazo hazijafikiwa na huduma ya majisafi kutoka ziwa Victoria zinafikiwa. Miji
hiyo ni Urambo, Sikonge na Kaliua. Mradi
huu unatekelezwa na kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 62.2 na unatarajia
kuhudumia wakazi zaidi ya 435,811. Aidha mradi huu utahudumia vijiji vyote
vinavyopitiwa na miundombinu ya mradi na kuleta uhalisia wa mawazo ya Waziri
Aweso ya kutompita mwananchi yeyote wa mkoa wa Tabora aliyeko katika eneo la
mradi.
Mhandisi Mayunga anasema kwa sasa
huduma ya maiisafi na salama katika Manispaa ya Tabora imefika asilimia 95 na
bado wanaendelea kusambaza miundombinu ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikiwa
wananchi kwa asilimia mia moja.
Anakiri kuwepo na changamoto ya
huduma ya maji katika baadhi ya miji anayoihudumia ambayo ni mji wa Sikonge
ambao kwa sasa huduma hiyo imefikia asilimia 42.5. Mji wa Urambo uko asilimia 24.5
na asilimia 50 katika mji wa Kaliua.
“Niwahakikishie wananchi wa
maeneo yote hayo kwamba taabu wanayopitia sasa ni ya muda tu kwani mradi huu
unategemea kupandisha huduma ya maji hadi kufikia asilimia 95. Tuombe uzima
tu.” Mkurugenzi Mhandisi Mayunga anasema
Kuona ni kuamini. Kutoka ofisini
kwa Mkurugenzi wa TUWASA safari yangu imeniwezesha kwenda hadi pori la Kijiji
cha Maswanya Wilayani Uyui ambako mkandarasi kampuni ya Mega Engineering and
Infrastructure LTD anaendelea na shughuli ya kutandaza mabomba mradi wa maji wa
miji 28. Safari hii siko peke yangu. Nimeambatana na Mkurugenzi Mhandisi Mayunga.
Pamoja na kwamba sikubahatika kuonana na msemaji wa kampuni inayotekeleza mradi,
kazi inaonekana kwenda kasi kwani kazi ya kuchimba mitaro inakwenda sambamba na
kazi ya kutandaza mabomba.
Mhandisi Mayunga ananihakikishia
kuwa yeye binafsi amezungumza na
mhandisi mshauri kampuni ya WAPCOS na mkandarasi. Pia waziri Aweso amezungumza
nao na kuwataka wakamilishe mradi kwa wakati kwani hakutakuwa na muda wa nyongeza.
Anasema zama za kurudi mezani
kuanza kuzungumza na mkandarasi kuongeza muda wakati yeye mwenyewe aliahidi
kuikamilisha kazi katika muda uliopangwa zimeisha. Lazima kazi ikamilike kwa
wakati. Wananchi wapate huduma.
Kila laheri wananchi wa Tabora. Kila laheri Sekta ya Maji. Muendelee kunena na kutenda. Taifa linawategemea katika kumtua “mama ndoo ya maji kichwani”. Kweli kuona ni kuamini, mapinduzi ni makubwa, na hongera na pongezi kwa wote, manake usipokuwa na shukrani hata mazuri unayaharibu.




Comments
Post a Comment