Mwalimu JK Nyerere, karibu Tena Butiana. Uyaone ya Aweso

 


Mpendwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Pole kwa majukumu mapya uliyonayo huko Peponi. Lengo langu kuu ni kukupa simulizi ya kinachoendelea katika sekta ya maji huko jimboni kwako lakini nimeona vema nianze kukupa pole kwa majukumu mapya kutokana na Imani yangu ambayo sina hakika kama iko sahihi kwamba kwa wachapa kazi kama wewe mnapoiaga dunia, Mwenyezi Mungu anawapa majukumu mengine ili muendelee kuijenga jamii katika ulimwengu huo mpya. Naomba nisamehewe kama fikra zangu haziko sahihi lakini niendelee kuaminiwa kwamba uliondoka wakati watanzania wengi tungali tunakuhitaji

Mpendwa Baba wa Taifa. Mimi ni mtanzania mwenzako ambaye nimekuwepo katika kipindi ukiiongoza nchi hii. Nimekuwepo nikiwa mmoja wa wakazi wa Mkoa wa Mara katika Kijiji cha Nambaza wilaya ya Bunda. Nikiri kwamba sikupata fursa ya kuwa miongoni mwa chipukizi uliokuwa ukituita kuja kukusaidia kuvuna mazao yako hapo Butiama. Pengine hiyo ingenipa fursa ya kukaa karibu na wewe na kuchota hekima yako.

Utakumbuka kwamba wakati wa mavuno ulikuwa ukituita vijana wa chipukizi kutoka sehemu mbalimbali mkoani hapo kuja kukusaidia kuvuna mazao. Si kwamba sikupenda kushiriki katika kazi hiyo njema isipokuwa walimu wangu waliokuwa wakiunda vijana wa chipukizi hawakuniona kwamba nina sifa hiyo.

Wao walidhani mimi ni goigoi lakini nikuhakikishie kwamba huo ulikuwa mtazamo wao. Mimi leo hii ni shujaa na mchapa kazi mzuri. Ukitaka uhakika wa hili muulize kijana aliekuwa kiongozi mkuu wa Scout, Innocent Sabato Nanzaba ambaye sasa ni Katibu wa CCM moja ya mikoa huko Unguja. Namtaja huyu kwa sababu nafahamu alikuwa na nafasi ya kukaa karibu na wewe katika shughuli mbalimbali wakati huo akiwaongoza vijana wote wa scouti huko Wilayani Bunda akitokea hapo kijijini kwetu.

Mpendwa Baba wa Taifa. Licha ya kuzaliwa huko mkoani Mara katika Jimbo la Mwibara ambalo wakati huo lilikuwa sehemu ya jimbo la Bunda, nilipata nafasi ya kuishi jimboni kwako katika Kijiji ha Kiabakari wakati huo likiitwa jimbo la Musoma vijijini. Uzoefu huu na utu uzima wangu umeniwezesha kufahamu baadhi ya masahibu waliyokuwa wakiyapata wakazi wa mkoa wa mara na hasa jimboni kwako kikiwepo Kijiji chako cha Butiama. Fursa hii ndiyo inayonipa nafasi ya kukusimulia hali inayoendelea sasa baada ya miaka kadhaa tangu utuage watanzania.

Mpendwa Baba wa Taifa. Utakumbuka vizuri kwamba uliacha mradi wa maji uliokuwa ukianzia Kijiji cha Mugango kuelekea Butiama kupitia kiabakari? Sikuwahi kukuambia lakini leo nikusimulie kwamba malalamiko ya wananchi wa kiabakari katika miaka hiyo ya 1990 wakati ambao ulikuwa umeshastaafu uongozi ilikuwa ni kwamba mradi huo umechakaa wewe huchukui hatua ya kuwaambia viongozi walioko serikalini ili wafanye haraka kuurekebisha. Jambo lililokuwa wazi ni kwamba kweli mradi ulikuwa umechoka kwelikweli. Maji yalikuwa yakitoka mara chache sana.

Kwa waliokuwa wakielewa msimamo wako walijipa majibu wenyewe kuwa hiyo ni tabia yako na msimamo wako wa kutotaka kuvutia maendeleo kwenye maeneo yako. Zaidi ulilenga maendeleo ya nchi nzima hasa kwa waliokuwa na mahitaji zaidi. Mfano wa wazi ulikuwa Barabara ya kuja kwako kutokea barabara kuu ya Mwanza Musoma.

Nakumbuka hadi unaiaga dunia, kutoka pale Nyamisisi Kiabakari, tulikuwa tukikata kona kuikamata barabara ya kuja Butiama nyumbani kwako tunaanza kukulaumu kwa nini barabara imechoka hivyo na wewe uko kimya tu. Tulikuwa tukikuona unapita na gari lako kimyakimya tunabaki kukushangaa. Tulikuwa tukijilinganisha na wenzetu wa mikoa ya kaskazini ambao tuliamini wana maendeleo kwa sababu viongozi wao waliokuwa chini yako waliamua kupeleka fursa huko kwao jambo ambalo wewe hukutaka kulifanya.

Majibu haya nilikuja kuyapata majuzi wakati nilipomsikia Mhe. Sospeter Mhongo Mbunge wa Jimbo la Msoma vijijini akisimulia kwamba uliwahi kumwambia kwamba wananchi wanakata mabomba na kusababisha wewe na wananchi wengine wa Butiama wakose maji. Mheshimwa Muhongo alitoa maelezo haya akiwaeleza wajumbe wenzake wa iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulika na maji wakati walipotembelea mradi Mpya wa maji wa Mugango-Kiabakari Butiama. Alisema wewe ulikuwa ukiishauri serikali isilenge kufikisha maji Butiama bila kuhakikisha wananchi wanaopitiwa na miundombinu hiyo wanapata huduma hiyo.

Mpendwa baba yetu. Leo ni zaidi ya miongo miwili tangu umetangulia mbele ya haki. Naomba nikupe siri kwamba sasa sekta ya maji imempata mchezaji. Msemo wa Waswahili kwamba upele umepata mkunaji umetimia. Sasa hivi serikali yako uliyoipenda inaongozwa na mwanamama Samia Suluhu Hassan. Sina shaka ulimuacha akiwa ameianza siasa lakini hakuwa katika nafasi za juu zaidi. Huyu Mama kaamua sekta ya maji kumpa bwana mdogo machachari kweli kweli anaitwa Jumaa Hamidu Aweso.

Huyu Aweso ni Mbunge wa Pangani. Alianza kama Naibu Waziri wa Maji akiwa chini ya Waziri Mbarawa, kisha akapewa nafasi ya uwaziri. Wakati anapewa madaraka kulikuwa na lawama lukuki za changamoto ya huduma ya maji sehemu mbalimbali nchini. Alipoingia madarakani tu akatangaza kuwa wizara yake ni Wizara ya maji si Wizara ya ukame.

Akasema atahakikisha Wizara hiyo inatoka kuwa wizara ya Kero na kuwa wizara ya kusuluhisha kero za wananchi. Akawa na kawaida ya kusimama jukwaani anatukumbusha kitabu cha Tenzi za Rohoni, wimbo namba 22 usemao ‘Unapozuru wengine usinipite mwokozi’. Akasema wizara yake itahakikisha haimpiti mtanzania yeyote katika kuhakikisha anafikiwa na huduma ya majisafi na salama. Tulidhani ni masihara ya wanasiasa lakini sasa tunayaona wazi.

Licha ya kuwa mchapa kazi ambaye hakai ofisini Kijana Aweso amekuwa na maamuzi ya haraka ya kuhakikisha anasikia shida na vilio vya wananchi. Hii imemfanya awe na sifa njema kwa kila jamii anayoifikia na hivyo kuwa miongoni mwa mawaziri ambao wanasifika zaidi kwa utatuaji wa haraka wa shida za wananchi.

Utendaji huu uliotukuka ndiyo unanipa nafasi ya kukusimulia hilo fupa la mradi wa Mugango wa kiabakari lilikuwa likifanya wananchi wakulaumu kwamba hujataka kulichukulia hatua.  Chini ya Rais Samia kupitia waziri Aweso mradi huo umeanza kujengwa upya kwa kuwekeza zaidi ya shilingi Bilioni 70. 5

Kile kilio chako cha kutaka wananchi wote wanaopitiwa na mradi huo wapate huduma kimepatiwa majibu. Chini ya Waziri Aweso mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu jumla ya vijiji 39 vinavyopitiwa na miundombinu ya mradi vitapata huduma ya majisafi. Hii itafanya wakazi takribani 233,000 kupata huduma kupitia mradi huu ambao umesanifiwa uwe na uwezo wa kuhudumia wananchi hadi mwaka 2040. hii inamaanisha kwamba hata ongezeko la wananchi watakaokuwepo kwa miaka hiyo, bado wataweza kupata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Mpendwa Baba wa Taifa kwa mapenzi makubwa niliyonayo kwako ninayo mengi ya kukusimulia jinsi nchi inavyokimbia katika masuala mbalimbali ikwemo sekta ya maji. kwa vile leo ni siku ya kukumbuka naomba niishie hilo moja. Siku nyingine nitakuwa na mengi yenye kukumbusha ulivyoweka misingi imara ya uongozi wa Nchi. Upumzike kwa amani. Mpendwa Baba wa Taifa.

Comments

Popular posts from this blog

Ujenzi wa Mabwawa kusaidia kuondoa changamoto ya maji Dodoma

Wataalamu Sekta ya maji shirikishaneni maarifa – Naibu Waziri Maji

Katibu Mkuu Wizara ya Maji asisitiza matumizi ya mfumo wa taarifa za sekta ya maji (Maji App)