Jamii ishirikishwe katika masuala ya maji - Aweso
Picha mbalimbali za Waziri wa Maji Mhe. Jumaa aweso akizungumza katika kikao cha mafunzo kwa Wakurugenzi na Menejimenti za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amezindua Bodi za Mamlaka za Maji Nchini na kuwataka viongozi wa Sekta ya Maji kuhakikisha wanashirikiana na wadau wengine katika hatua mbalimbali ili kuhakikisha Sekta ya Maji inasonga mbele.
Kabla ya kuzindua Bodi hizo Mhe. Aweso amefungua kikao cha mafunzo kwa Wakurugenzi na Menejimenti za mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira ambapo amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Prof. Jamal Katundu kuhakikisha bodi hizo zinakuwa mkono wa wizara na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa, viongozi wa Serikali, wafanyabiashara na watumishi wastaafu waliobobea katika masuala ya maji.
"Hatuwezi kufanya kazi peke yetu. Lazima tuhakikishe tunashirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea" Mhe. Aweso amesema na kuongeza kuwa lengo ni kufikia upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kwa asilimia 85 na mijini asilimia 95, na kupita kiwango hicho ili kuwafikia wananchi “kumtua mama ndoo ya maji kichwani”.
Amesema hivi sasa zoezi la utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maji linaendelea vizuri na jambo la kuangalia ni
kuhakikisha utoaji wa huduma za uhakika na taarifa kwa wateja pale inapotokea
hitililafu katika uzalishaji wa maji.
Akizungumzia suala la upotevu wa
maji (NRW) amezitaka bodi kufuatilia kwa kina kuhusu mivujo na kiwango cha maji
kinachopotea ili kuona uhalisia wa taarifa kwa sababu inawezekana maji
yanatumika bila kulipiwa.
Mafunzo hayo yameshuhudia bodi za
wakurugenzi za mamlaka za maji 25 zikizinduliwa na baadhi ya mamlaka za maji
zikipandishwa madaraja kuendana na vigezo ikiwamo vya utoaji huduma na kumudu
kujiendesha.






Comments
Post a Comment