Wakazi wa Igegu Waishukuru Serikali kuwafikishia huduma ya Maji
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja akilitazama tenki la mradi wa maji kijiji cha Igegu
Tanki la mradi wa maji IgeguWakazi wa Kijiji Cha Igegu Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu wameonyesha kujawa na furaha na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufikishiwa mradi wa maji katika Kijiji Chao kwa mara ya kwanza.
Akizungumza katika ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja Kijiji hapo ndugu Suzana Mangalu Mng'ela amesema kwasasa wanaenda kuondokana na changamoto zote zilizowakabili hapo awali.
"Tunaishukuru sana Serikali kwa mradi huu wa maji, tulifata maji mbali sana mpaka Kijiji Cha Dutwa, lakini sasa tunatumaini kubwa na mradi huu utakapozinduliwa tutaweza kufanya shughuli nyingine za maendeleo na nyumbani ambazo awali hatukuweza kwajili yakutafuta maji" ameeleza ndugu Suzana.
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Igegu, ndugu Samweli Ezekiel amepongeza jitihada za Serikali kuwafikishia maji wananchi wa Igegu na sasa wanaimani kubwa ya kupata mafanikio zaidi Kwa kuongeza shughuli za maendeleo.
Mhandisi Cyprian Luhemeja, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, ametoa maagizo kwa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Simiyu kuhakikisha ndani ya mwezi wa nane mradi huo wa maji kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
"Wananchi Hawa wanahitaji Maji, pamoja na mradi mkubwa wa Maji Simiyu unaoendelea mradi huu wa maji Igegu ni jitihada za Serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji, na sasa nimuagize Meneja wa RUWASA Mkoa kabla ya mwezi wa nane kuisha mradi huu uwe umekamilika na kutoa huduma" ameeleza Mhandisi Luhemeja.
Mradi wa maji Kijiji Cha Igegu unaogharimu kiasi cha shilingi milioni 561 umehusisha ulazaji wa Bomba kwa umbali wa Km 21, ujenzi wa vituo vya kuchota maji 17, ujenzi wa tenki la maji Lita 135,000 na utahudumia zaidi ya wakazi 5700 wa Kijiji hicho na maeneo jirani.


Comments
Post a Comment