"Tujitume katika kazi" Luhemeja
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja amewataka wafanyakazi wote wa Mamlaka za maji pamoja na RUWASA na Watumishi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria kujituma zaidi katika kazi.
Mhandisi Luhemeja amewaasa Watumishi wote kuwa ni lazima kufanya kazi kwa bidii na kujituma Ili kufikia malengo ya Wizara kiujumla ya kila mwananchi kupata huduma ya majisafi na salama. Amesema hayo akihitimisha ziara ya kikazi mkoani Mara.
"Kufanya kazi ya kutoa huduma ya maji ni jambo la kuheshimika sana, niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya katika Mkoa wa Mara. Hali ya utoaji huduma inaridhisha, naomba sasa tukaongeze juhudi Ili tutimize malengo yetu" Mhandisi Luhemeja amesema
Aidha Mhandisi Luhemeja alitumia nafasi hiyo kuagiza Mamlaka za maji mkoani Mara kumaliza changamoto ya upotevu wa maji kwa kupambana na wizi wa maji.
Kwa upande wake Mbunge wa Musoma Mjini Mhe. Vedastus Mathayo amewapongeza watendaji wa Mamlaka za Maji Mkoani Mara kwa kujituma na kuhakikisha huduma inaimarika kila kukicha.
"Niseme kweli hali ya huduma hasa Musoma mjini ni nzuri sana, upatikanaji wa maji ni zaidi ya asilimia 95, watendaji wa Mamlaka hizi wanafanya kazi vizuri na hatupokei malalamiko kuhusu kazi yao" Mhe. Mathayo ameainisha
Ameongeza kuwa anaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa sikivu na kuwapatia fedha za miradi ya maji kwa wakati huku akisema sekta ya maji inaheshimisha sana Mkoa wa Mara.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi mkoani Mara anategemea kuanza ziara ya kikazi Mkoani Shinyanga kuanzia Tarehe 20-22 Julai, 2023.





Comments
Post a Comment