Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja akikagua tenki la maji la mradi wa maji BugaramaMradi wa maji wa Bugarama unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7 upo mbioni kukamilika na kuleta tija katika jamii ya wanufaika wa mradi huo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja amekagua ufanisi wa utekelezaji wake na kuridhishwa na kazi iliyofanyika.
"Nitoe pongezi kwa kazi nzuri inayoendelea hapa katika mradi huu wa maji wa Bugarama, Mkandarasi anafanya vizuri na ameahidi ifikapo tarehe 21 Septemba, 2023 kazi itakuwa imekamilika" Mhandisi Luhemeja amesema.
Amewataka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA) kuhakikisha usimamizi mzuri wa fedha zitokanazo na miradi hii kwa kuingia katika mifumo rasmi ya usimamizi ya Serikali Ili kuepuka dalili zote za upotevu wa fedha.
"RUWASA sasa wanatakiwa kubadilisha fikra katika utoaji wa huduma, badala ya kuwaza kuweka vituo vya kuchotea maji na kuunda vikundi vya jamii ya watumia maji wanapaswa kufikisha maji katika makazi ya wananchi " Mhandisi Luhemeja amesema
Mhandisi Mashaka Sita ambaye ni mratibu wa mradi huo ameeleza kuwa kutokana na ongezeko la watu katika eneo la Bugarama na vijiji vya pembezoni waliamua kutekeleza mradi Ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa maeneo hayo.
"Mradi huu utakamilika mwezi Septemba 2023, na utahudumia vijiji vinne vya Bugarama, Ilogi, Lwabakanga pamoja na Kakora namba 9 vyenye wakazi zaidi ya 25,000" Mhandisi Sita ameainisha.


Comments
Post a Comment