Mkandarasi wa mradi wa majitaka Chato atakiwa kuongeza kasi
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja, amekagua mradi wa majitaka wa Chato mkoani Geita na kumtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kampuni ya Peritus Exim Private kuongeza kasi ya utekelezaji na ukamilike ifikapo Aprili 2024.
"Niwapongeze kwa kazi iliyofanyika lakini Mkandarasi anatakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huu Ili wananchi waanze kuona matokeo yake. Mkandarasi ahakikishe mradi unakamilika ifikapo Aprili 2024" Mhandisi Luhemeja amesema.
Ameongeza kuwa ifikapo mwezi Novemba 2023 Mkandarasi huyo awe amekwisha nunua magari mawili ya uondoshaji majitaka na yaanze kutoa huduma hiyo katika wilaya ya Chato
"Gharama za uondoshaji majitaka hapa Chato ni kubwa mno, wananchi wanalazimika kutafuta magari ya utoaji huduma kuja hapa Chato kutoka Mwanza kitu ambacho sio sahihi, tumekubaliana na mkandarasi ifikapo Novemba 2023 magari hayo yawe yamenunuliwa na kutoa huduma" Mhandisi Luhemeja ameainisha.
Naye Mkandarasi, ameeleza kuwa wamepokea maelekezo hayo na kuhakikisha yanafanyiwa kazi kwa wakati.
Mradi wa majitaka wa Wilaya ya Chato utekelezaji wake umefika asilimia 25 na utahusisha ujenzi wa mabwawa matano yakuchakata majitaka na gharama yake ni kiasi cha shilingi bilioni 1.5



Comments
Post a Comment