Waziri Mkuu Awataka Wizara ya Maji kushirikiana na wadau wa sekta ya maji

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) akikagua shughuli zinazofanywa na Wadau mbalimbali kwa kushirikiana na WaterAid Tanzania alipowasili katika ukumbi wa Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Uzinduzi wa Mkakati Mpya wa Nchi wa WaterAid Tanzania 2023-2028 na Maadhimisho ya Miaka 40 ya WaterAid Nchini Tanzania
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Mkakati Mpya wa Nchi wa WaterAid Tanzania 2023-2028 na Maadhimisho ya Miaka 40 ya WaterAid Nchini Tanzania.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) akimkabidhi Naibu Waziri wa Maji Mhandishi Maryprisca Mahundi (Mb) zawadi ya kumbukumbu wakati akizinduza Mkakati Mpya wa Nchi wa Asasi ya WaterAid Tanzania 2023-2028

Mhe. Majaliwa akikata Keki wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa WaterAid Tanzania


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ameitaka Wizara ya Maji ishirikiane na wadau mbalimbali wa sekta ya maji ili kutengeneza na kutekeleza mwongozo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya Maji.

Agizo hilo amelitoa wakati akizindua Mkakati Mpya wa Nchi wa Asasi ya WaterAid Tanzania 2023-2028 na Maadhimisho ya Miaka 40 ya Asasi hiyo nchini Tanzania iliyofanyika jijini Dar es Salaam. 

Amesema yapo mafanikio mengi yaliyoletwa na Wizara ya Maji lakini bado inatakiwa kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinafikisha huduma endelevu, jumuishi na salama ya majisafi, usafi wa mazingira na usafi binafsi kwa Watanzania wote.

Aidha, Wizara ya Maji kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Maji ihakikishe miradi yote inayoendelea katika Sekta ya Maji inatekelezwa kwa ufanisi na inakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha. Amesema hiyo itasaidia kufanikisha na kuharakisha uwekezaji katika Sekta ya Maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) akimwakilisha Waziri wa Maji amewashukuru Asasi ya WaterAid Tanzania kwa kuwa tayari kusaidia Sekta ya Maji nchini. Amesema utekelezaji wa Mpango uliopita umewezesha ujenzi wa idadi ya miradi 73 inayojumisha miradi 14 ya maji, miradi 57 ya miundombinu ya WASH kwenye shule na vituo vya kutolea huduma za afya, na miradi 2 ya miundombinu ya udhibiti majitaka.

Utelekelezaji wa miradi hiyo umepelekea wananchi kupata majisafi na salama, vituo vya afya 35 kupata huduma ya maji na shule 30 zimepata miundombinu ya WASH ikiwemo miundombinu ya uvunaji maji ya mvua.

Awalia akitoa salam za ukaribisho Mkurugenzi Mkazi wa Asasi ya WaterAid Tanzania. Anna Tenga Mzinga ameshukuru ushirikiano mzuri ambao wameupata kwa muda wote tangu wameanza kazi nchini Tanzania. Amesema kwa miaka 40 iliyopita Asasi hiyo imewafikia watu milioni 8 moja kwa moja kwa huduma ya maji safi, kuwapatia watu 800,000 vyoo bora, na kuwafikia watu milioni 26 kwa uhamasishaji wa usafi wa mazingira wanaofanya kazi katika Mikoa 11 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) akimkabidhi Naibu Waziri wa Maji Mhandishi Maryprisca Mahundi (Mb) zawadi ya kumbukumbu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mkakati Mpya wa Nchi wa Asasi ya WaterAid Tanzania 2023-2028 na Maadhimisho ya Miaka 40 ya Asasi hiyo nchini Tanzania

 

Comments

Popular posts from this blog

Ujenzi wa Mabwawa kusaidia kuondoa changamoto ya maji Dodoma

Wataalamu Sekta ya maji shirikishaneni maarifa – Naibu Waziri Maji

Katibu Mkuu Wizara ya Maji asisitiza matumizi ya mfumo wa taarifa za sekta ya maji (Maji App)