Mwisho wa Dola ya Marekani huu hapa
Nimeingia katika maktaba yangu ya historia. Maktaba hii
inahusisha yale niliyoyasoma kuanzia kidato cha kwanza hadi elimu ya Chuo Kikuuu.
Nauona mwisho wa taifa linaitwa Marekani (USA). Imani yangu ni kwamba mwalimu
wangu wa historia hasa aliyenifundisha kidato cha kwanza hakunidanganya
kuniambia kwamba jambo lolote linaweza kuangaliwa katika mtazamo wa kihistoria.
Alisema historia inasaidia kujifunza yanayotokea leo, kutokana na yale
yaliyowahi kutokea. Alisisitiza kwamba elimu hiyo itanisaidia kuepuka ili
nisije nikafanya makosa kama waliyoyafanya wengine. Sina shaka Mwalimu wangu Magudila
Mgeta wa Bwasi Sekondari miaka ya tisini tukizoea kumuita kwa jina la utani ‘TX’
alikuwa sahihi.
Maarifa ya mwalimu TX yananipa
jicho la kukitazama Kinachoendelea katika mapambano kati ya Urusi Na Ukraine.
Sasa inaelekea ni vita kati ya Urusi na Washirika wake dhidi ya NATO
wakiongozwa na taifa kubwa zaidi kiuchumi duniani, taifa la Marekani. Urusi
naye amekataa kuwa peke yake. Amewapata wapambe wake wakiongozwa na China taifa
ambalo linatajwa kukua zaidi kiuchumi duniani. Mpambano huu umeigawa dunia. kila
mmoja amekuwa mtabiri. Wengine wakiutabiri mwisho wa Marekani na NATO kwa
ujumla. Wengine wakiutabiri mwisho wa Urusi. Sisi yetu macho lakini maktaba
yangu ya historia hainidanganyi. Inanikumbusha mengi.
USA na washirika wake wana nafasi
ya kujifunza kupitia sababu mbalimbali zilizowafanya wenzao wakapotea katika
ulimwengu wa mafahari wa Dunia. Shuleni tulifundishwa dola maarufu zilizobeba
simulizi ya wakati huo. Dola ya Ghana, Dola ya Mali, Songhai, Dola ya
Mwenemtapa. Asante na zingine nyingi.
Hizi dola ziliongozwa na watu maarufu,
huko kwetu majita wanawaita ‘Chikaka, Masika, Mwamba, Chitama Bhagegi’, (shujaa
asiyeshindwa). Hawa ni pamoja na Kaya Magha, wananchi wake wakimuita kwa jina
la utani kuoneshwa nguvu yake kubwa isiyoweza kushindwa na yeyote, Tunka
Manini. Walikuwepo akina Sundiata Keita. Mansa Kankan Mussa, Opuku Ware, Asante
Hene huko Assante Empire. Zote hizi
zlianguka kutokana na kujihusisha na masuala ya vita.
Narudia tena kuwa historia haidanganyi.
Historia haisemi uongo. Tengeneza fedha. Badala ya kutumia fedha hizo kutafuta
amani jifanye unaweza kupigana. Jifanye unaweza kumnyamazisha kila mtu.
Utatengeneza mabomu mpaka ya kupuliza kwa mdomo likaenda kuua mtu au kuangamiza
Kijiji, lakini vita haitakuacha salama. Utaua wengi. Utanyamazisha wengi lakini
iko siku utajuta, utakumbuka nguvu uliyokuwa nayo. Utajikuta umechelewa, wakati
huyo wenzako watakuwa wamechukua nafasi. Haya ndiyo yaliwakuta wote. Mobute
Tseseseko Kuku Ngembu wa Zagamba huko Zaire, Idd Amin huko Uganda, Tsar
Nicolaus huko Urusi ya miaka hiyo.
USA na washirika wake wakumbuke enzi
za Uingereza akiwa Bingwa na shujaa wa dunia (Super Power of the World). Historia
inasema vita hizi hizi ndizo zilimuondoa katika nafasi ya super power wa dunia.
Taifa la Marekani lililochagua kujitenga na vita likachukua nafasi.
Akumbuke kipindi alichopitia
Uingerea akijitamba kwamba hakuna saa jua liliwahi kuacha kuangaza ardhi ya
uingereza, (The Sun Never Sets on British Empire). Ujumbe huu ulikuwa kweli kwa
sababu Uingerea alikuwa ametawanyika dunia nzima. Kama jua linazama Uingereza
koloni lake la Afrika mashariki ni mchana. Kama Afrika Mashariki ni usiku
koloni lake huko Amerika ilikuwa ni mchana. Huyu ndiye aliyewahi kuifanya Marekani
ya sasa kuwa koloni lake. Waingereza wakafanya kosa la kujiingiza kwenye vita
ya kwanza na ya pili ya Dunia. Marekani akajitenga, akawa ni muuzaji wa silaha
kwa mafahari walioko vitani, walipoishiwa bado akawa ni mkopeshaji mkuuu. Mbinu
hiyo iliyopitia katika mpango wa mtaalamu wa uchumi wa Marekani akijulika kwa
jina la Marshal (Marshal Plan) ikalifanya taifa la Marekani kuwa kubwa. Baada
ya vita, Uingereza bingwa wa dunia badala ya kupambana kuimarisha uchumi wake,
akawa na nguvu kubwa kulipa madeni ambayo yalikuwa yakimuendea marekani ambaye
alitumia fursa hiyo kuimarisha uchumi wake. Uingereza ikapoteza umaarufu,
Akakubali kutoa fursa kwa Marekani. Historia na waswahili tunamwambia Marekani
kwamba hakuna marefu yasiyokuwa na ncha.
Iliwahi kuwepo dola ya Kirumi.
Hii ilitawala karibia ulaya yote hadi baadhi ya mataifa ya Afrika yaliyoko
kaskazini, Misri, Libya na Algeria. Yesu alizaliwa ndani ya dola hii wakati huo
wakiwemo magavana mbalimbali kama Ponsio Pilato aliyekuwa akitawala yudea.
Jeuri ya Mamlaka na nguvu kubwa kiuchumi ikawapa nafasi ya kutoa hukumu ya Yesu
Kuuawa msalabani. Nani aliyeamini Dola ya kirumi itafikia mwisho? Nani aliamini
hawa wenye nguvu ya kumhukumu Yesu wangepoteza umaarufu? Vita ikaibua upinzani ndani
ya himaya, watu wakagawanyika. Wakashindwa kuwaamini watawala kama ambavyo
Wamarekani sasa wanasema angekuwa Trump Marekani Isingeingia kwenye huu
mgogoro. Kazi ikawa nyepesi kabisa kwa dola ya Ottoman kuchukua nafasi baada ya
kuvamia baadhi ya maeneo ya dola ya Rumi.
NATO wakumbuke nguvu kubwa
waliyokuja nayo dola ya Ottoman. Hii iliojitanua. Wakawa mwamba wa dunia. Sehemu kubwa ya maeneo yaliyokuwa chini ya
dola ya Rumi yakawa chini ya Ottoman. Wakasambaa, wakazichukua nchi za Afrika Kaskazini
kama vile Libya, algeria, Syria, Misri. Dola ikatanuka hadi kusini mashariki
mwa Ulaya kwenye nchi kama hungary, Ugiriki, Ukraine. Ikaenda hadi uarabuni.
Ubabe na kujiona wananguvu zaidi, kupenda vita kukaifanya dola hiyo kufikia
mwisho, leo hii ni historia.
Ukiangalia katika uhalisia wa
dunia inavyokwenda sasa hivi. Marekani ni zaidi ya nchi. Ni dola kubwa duniani.
Imetawanya nguvu zake kila sehemu duniani. Imeweka vituo vya kijeshi kila
mahali. Imekuwa na nguvu ya kushinikiza masuala mbalimbali yakiwemo ambayo nchi
za kiafrika zinayatafsiri kwamba ni kinyume na miongozo ya kimaadili na kidini.
Pamoja na nguvu hiyo ambayo
imedumu kwa muda mrefu taratibu mambo yanaanza kubadilika. Nguvu yake ya
ushawishi wa dunia kijeshi, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni inaendelea
kuporomoka. Wamejigawa kisiasa. Wengine wanaanza kumwelewa Donald Trump kupitia
slogan yake ya kwamba ‘Make America Great Again’. Wanaamini kwamba nguvu ya
Marekani inaendelea kupotea kila kukicha.
Kidodo kidogo tunaanza kuuona
muungano wa kifedha. Mataifa yanaanza kutafuta mbinu za kupunguza utegemezi wa
dola. Mataifa kama China, India, Afrika Kusini na Russia wanafikia makubaliano
ya kuachana na matumizi ya dola. Ni
suala la muda tu. Historia itaweka wazi tutaanza kusema lilikuwepo dola kubwa
la Marekani kama tunavyosema lilikuwepo dola kubwa la Uingereza. Lilikuwepo dola
la Rumi.


Comments
Post a Comment