Wadau wa Sekta Mtambuka watakiwa kuwekeza Zaidi kwenye utunzaji na uhifadhi wa rasilimali za maji
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandishi Anthony Sanga
amelitaka Jukwaa
la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi na
Uendelezaji wa Rasilimali za Maji
kuwekeza Zaidi kwenye utunzaji na uhifadhi wa Rasilimali za Maji
ili kuwezesha upatikanajni wa maji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii
na kiuchumi.
Wito huo ameutoa leo kupitia hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa vikundi kazi vya jukwaa hilo iliyosomwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Maji ya Taifa Mhandisi Mbogo Futakamba jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Sanga amesema Serikali inatekeleza sera ya Tanzania ya Viwanda ambayo kwa kiasi kikubwa inahitaji umeme ambao msingi wake mkubwa ni maji.
Picha ya pamoja ya Baadhi ya wajumbe wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji
“Tanzania ya viwanda inategemea
upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu ambao kama mnavyofahamu,
umeme unaotokana na nguvu ya maji ni wa gharama nafuu zaidi. Kwa mfano, gharama za uzalishaji umeme wa nguvu za maji shilingi
13 kwa uniti, umeme wa gesi asilia shilingi
129 hadi 153 na kwa mafuta ya dizeli shilingi
546 hadi 675. Kwa kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Nyerere kwa
ajili ya kuzalisha umeme wa maji kiasi cha megawati 2,115 ambapo Mradi huu
ukikamilika zaidi ya 70% ya umeme wote nchini utakuwa ni wa maji. Hivyo hatuna
budi kuhakikisha rasilimali maji inatunzwa na kuendelezwa” Amesema mhandishi
Sanga.
Aidha, ameagiza kila Kikundi Kazi katika
jukwaa hilo kiandae Mpango Kazi wa utekelezaji kila mwaka. Pia Mkakati wa
utafutaji fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zilizoainishwa ndani ya
Mpango.
Baadhi ya wajumbe wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka wakijadiliana masuala mbalimbali kuhusiana na utekelezaji wa majukumu yao
Jukwaa la Wadau
wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji limeundwa kwa lengo
la kukutanisha Wadau wa Rasilimali za Maji kujadili na kubadilishana uzoefu na
ujuzi ili kuboresha utendaji kazi na kuhakikisha usimamizi endelevu wa
Rasilimali za Maji kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na baadae. Jukwaa hilo lina
Wadau zaidi ya 100 wanaotoka katika Taasisi takriban 90 za ndani na nje ya
nchi.

Comments
Post a Comment