Bangi ni malighafi bora ya kuzalisha chuma.
Profesa George Wajackoyah mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha Roots Party nchini Kenya amevuta hisia za wengi katika mitazamo tofauti. Hoja kubwa iliyogusa wengi ni ahadi yake ya kuruhusu kilimo cha bangi iwapo atapewa nafasi ya kuwa Rais wa Kenya. Hili linamfanya afananishwe na mgombea wa urais nchini Tanzania kupitia chama cha CHAUMMA kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita Mhe. Hashim Spunda Rungwe, ambaye pamoja na ahadi zingine ilikuwa kupanua Bahari ya Hindi kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Profesa George WajackoyahNimevutiwa na hoja za mgombea huyu na kuamua kuandika Makala hii ambayo inatokana na mahojiano niliyoyafanya na mmoja wa wahadhili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Leonard Mwaikambo mwanzoni mwa mwaka 2013. Wakati huo alikuwa katika kitengo cha uhandisi wa viwanda vya nguo (Textile engineering) na upande wa ubunifu wa nguo na teknolojia (Textile Design and Technology). Kwa sasa sina taarifa zake zaidi.
Mahojiano hayo niliyaandikia Makala na kuichapisha kwenye gazeti la Mtanzania mwaka huo ikiwa na kichwa cha habari, “Serikali iruhusu kilimo cha bangi”
Msomi huyu alikuwa akiomba serikali iruhusu kilimo cha bangi. Hoja yake ilikuwa imetokana na utafiti alioufanya ndani na nje ya nchi na kubaini uwezekano wa mkubwa wa mti wa bangi kuzalisha malighafi ya chuma bora ambacho kinaweza kutumika kutengeneza vifaa mbalimbali. Anasema bodi ya kwanza ya gali la aina ya ‘Ford’ ilitengenezwa kwa kutumia nyuzi za mti wa bangi. pia zipo bidhaa nyingi ambazo zinauzwa sokoni na zimetengenezwa kutokana na mti wa bangi.
Shamba la bangi kabla ya kuteketezwa chini ya usimamizi wa polisi wilayani SumbawangaKabla ya kuanza kunieleza mazuri yaliyoko katika mti wa bangi Dkt. Mwaikambo alianza kwa kunipa historia ya Maisha yake kielimu kwamba alisoma Chuo kikuu cha Bolton fani ya teknolojia ya Viwanda vya nguo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam fani ya uhandisi (Mechanical Engeneering) kisha akaenda Italia na Uingereza ambako huko aliweza kuhitimu shahada ya tatu ya Udaktari.
Anasema katika hali ya kuthamini maarifa yaliyoko kwa wenzetu, ajabu aliweza kuiona akiwa katika hatua ya mwisho ya masomo yake.
“Wenzetu huko wanakuwa na watu ambao shughuli yao ni kuangalia wasomi katika vyuo mbalimbali ambao wanaonekana kuwa na maarifa ambayo yanaweza kuleta mchango katika kufanikisha maendeleo ya nchi zao. Nikiwa katika hatua ya mwisho ya masomo yangu, mmoja wa wataalamu wa chuo kikuu cha Warwick ‘University of Warwick’ Coventry huko uingereza aliniona. Akaniomba kufanya nao kazi baada ya kumaliza masomo katika Chuo Kikuu cha Bath huko huko Uingereza”.
Anasimulia kwamba Alikubali lakini kwa sababu ya uzalendo na matamanio yake ya kurudi Tanzania alikubali kusaini mkataba wa miaka miwili tu. Baada ya hapo akarudi kuitumikia nchi yake.
Anasema kilichokuwa kikimsukuma ni hamu ya kukubali kwamba amepata maarifa yanayoweza kuwa na mchango mkubwa katika serikali yake. Alirudi na kufanya kazi katika chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Wakati narudi nchini, moja ya mambo yaliyokuwa yakinisukuma na ambayo nilitamani kuyabadilisha kwa manufaa ya nchi ni kuhakikisha raslimali nyingi zilizoko hapa nchini zinabadilishwa na kutumika katika kuiendeleza nchi.” Anasema Dkt. Mwaikambo.
Moja ya eneo alilolifanyia kazi ni matumizi ya takataka katika kuzalisha bidhaa.
“Baada ya kufika hapa nikajikita katika kutafiti malighafi hizi ambazo tunaziona kwamba hazina thamani kama zinaweza kusaidia kubadilisha uchumi wa nchi. Nilizunguka sehemu mbalimbali Tanzania ambako sufi, pamba, katani, maweze, mpunga na takataka kama chupa za maji machafu, pumba za mazao mbalimbali, mataili mabovu yanatupwa, na vitu mbalimbali ambavyo vinaonekana kwamba ni takataka, kama vinaweza kubadilishwa kuwa malighafi ya kutengeneza bidhaa.
Utafiti huu ndio umenifikisha kuzalisha vitu vya thamani ya hali ya juu kabisa. Kwa kutengeneza mchanganyo wa utomvu wa korosho, Sufi, pumba za mpunga, nyunzi zinazo tokana na mti unaosemekana kuzalisha ‘bangi’ ndio nikaweza kutengeneza vitu hivi unavyoviona hapa”
Anaonesha mezani kwake ambako kuna vitu kama vipande vya mabati maarufu kama mabati ya South Afrika, sahani, mbao, vitasa vya milango, nyuzi, bomba za kupitishia nyanya za umeme, karavati za mitalo ya maji machafu pamoja na vitu vingi mabavyo anasema vyote hivyo kavitengeneza kwa kutumia matakataka yanayoonekana kutokuwa na thamani katika jamii.
Anautaja mti wa bangi (hemp plant) kama malighafi nzuri ambayo kama serikali ikiwa na njia muafaka itasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa kiwango kikubwa.
“Mti huu ambao nimeona kwenye vyombo vya habari ukiteketezwa, una urefu wa wastani mita tatu au futi 10 na unakuwa hauna matawi kwa wingi. Huu mti kama ninavyo fahamu hauna uwezo wa kuzalisha chemikali inayoitwa ‘Tetrahydrocannabinol’ ambayo ndiyo inasemekana kuwa ni kiashiria cha ulevi kwa binadamu.”
Anasema kwa utafiti wake, gamba la juu la mti wa bangi lina nyuzi ngumu kuliko hata chuma. Anasema uzi mmoja wa bangi ukiulinganisha na uzi wa chuma, uzi wa bangi ni mgumu zaidi.
Anasema bodi ya kwanza ya gali la aina ya ‘Ford’ ilitengenezwa kwa kutumia nyuzi za mti wa bangi. Anaishauri serikali iruhusu kilimo cha zao hilo la mti wa bangi isipokuwa iweke sheria ambayo itazuia matumizi mabaya ya malighafi hiyo. Anasema huo ndiyo utaratibu unaotumika nchi zingine zinazozalisha nyuzi zinazotokana na mti wa bangi (hemp fiber) kama vile Uingereza na nchi za Ulaya Magharibi. Tukifanikiwa katika hili naamani tutapiga hatua kubwa katika kuiendea dunia ya matumizi ya bidhaa ya ndani kwa maendeleo ya nchi.
Anasema Julai, 2005 alikutana na Mhe. Pius Ng’wandu wakati huo akiwa ni Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu kumuonesha kazi yake na ugunduzi aliokwisha ufanya. Anafurahi kwa mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka katika ofisi hiyo.
Bahati mbaya pamoja na heshima aliyoonyesha Waziri, jitihada zake ziliishia njiani kwani mwishoni mwa mwaka 2005 Mhe. Ng’wandu alimaliza kipindi chake. Uchaguzi uliofuata hakugombea tena. Hivyo tangu hapo serikali ilikuwa haijaonesha kuhitaji kuyafanyia kazi mawazo yake.
Katika matukio ambayo anakumbuka ni moja ya mwaliko alioitwa kuwasilisha ugunduzi wake huko Australia katika chuo kikuu cha Queensland Toowoomba. Hiyo ilikuwa Desemba mwaka 2008.
“Kwa kweli sikutegemea kama ningeweza kupata heshima niliyoipata. Baada ya kuwasilisha utafiti wangu, karibia wageni kutoka viwanda na vyuo mbalimbali walinifuata kila mmoja akihitaji kupata maelezo ya ziada juu ya matumizi ya takataka hizo. Hata shirika la utangazaji la Australia (ABC) likaja kunihoji na mahojianao hayo yako katika mtandao wao.
Mmoja wao alipata nafasi ya kunieleza kwamba katika dunia wanayoiona leo hii, baada ya maiak 50, malighafi hii ya chuma na madini tunayoyapata kutoka ardhini hayatakuwepo tena. Hivyo teknolojia hii ndiyo itakuwa ikifanya kazi. Hivyo wanauhitaji utaalamu huo ili kujiandaa na dunia ya miaka 50 badaye.
Pamoja na mambo mbalimbali Dkt. Mwaikambo alikuwa akiomba serikali iruhusu hata kwa gharama yoyote, wamfadhili avijaribu vifaa vyake hivyo katika mazingira yoyote.
“Waniwezeshe nijenge hata kijumba ndani ya eneo fulani ambalo linaweza kuwa la maonesho. Nitumie mabati yangu, milango yangu, vitasa vyangu, meza zangu, na vifaa vyote ambavyo vitakuwa katika teknolojia hii. Naamini baada ya hapo hatutahitaji tena kuagiza mabati Afrika Kusini. Kila kitu kitazalishwa hapa Tanzania.”
Sasa ni karibia miaka 10 tangu nilipofanya haya mahojiano. Mabadiliko yoyote ya kimazingira yaweza kuwepo lakini bado kuna hitaji la kuwatumia wataalam wetu katika ubunifu mpya.
Masuha8@gmail.com
0717697205
.jpg)



Comments
Post a Comment