MIRADI YA MAJI YA UVIKO 19 IKAMILIKE KWA WAKATI-NAIBU WAZIRI WA MAJI MAHUNDI
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi(Mb) amewataka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Simiyu kuhakikisha miradi yote ya Maji inayotekelezwa kupitia fedha zilizotolewa na serikali ikiwa ni Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19 inakamilka ifikapo mwishoni mwa mwezi April mwaka huu.
Naibu Waziri,Mahundi amesema hayo wilayani Busega mkoani Simiyu alipotembelea
ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye mita za ujazo 50 kwenye mnara wa mita
15 katika kijiji cha Badugu.
Amesema hakuna sababu ya Mkandarasi kushindwa kukamilisha
kazi kwa muda huo kwani fedha kwa ajili ya miradi hiyo ipo kinachotakiwa ni
kufanya kazi kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu na kufuata taratibu za kuomba
pesa na kwamba Wizara ya Maji hawana
urasimu wowote juu ya utoaji wa fedha za miradi hiyo.
Aidha, amemtaka Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo Kampuni
ya Jonta Investiment ya Mjini Shinyanga kufanya kazi usiku na mchana ili mradi
ikamilike kwa muda uliopangwa.
"Rais ametoa fedha nyingi kwenye Wizara ya Maji ili
kuondoa kadhia kwa wananchi na kufikia azma yake ya kumtua mama ndoo kichwani,
hivyo mimi kwa kushirikiana na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso hatutakubali
mtu yeyote kukwamisha miradi",alisema Mahundi.
Awali Kaimu Meneja RUWASA Wilaya ya Busega, Mhandisi Daniel
Gagala akisoma taarifa ya Utekelezaji wa
Mradi huo amesema kiasi cha Sh 317,923,663
zitatumika hadi mradi utakapokamilika.
Amesema hadi sasa kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa
tenki, Ujenzi wa vituo tisa vya kuchotea maji, Ujenzi wa nyumba ya mambo na
ununuzi wa bomba.
Wizara ya Maji ilipokea jumla ya shilingi Bilioni 139.4 kutokna
na Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19.
Fedha hizo zinatumika kutekeleza miradi ya maji sehemu mbalimbali nchini.
Comments
Post a Comment