Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Amos Cheptoo kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa benki hiyo na kuwa sehemu ya mafanikio makubwa yanayopatikana katika Sekta ya Maji nchini Tanzania.
Waziri Aweso ametoa shukrani hizo na kuahidi ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Bw. Cheptoo katika kikao kilichofanyika jijini Arusha kwa lengo la kujadili maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Jiji la Arusha wenye thamani ya Sh. bilioni 520 ambazo sehemu ya fedha hizo kiasi cha Dola za kimarekani 210,962,581 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Akizungumzia mafanikio yanayotarajiwa baada ya kukamilika kwake, Aweso amesema mradi huo wenye lengo la kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira jijini Arusha na baadhi ya maeneo ya wilaya ya Arumeru utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 40 kwa siku mpaka lita 200 kwa siku kufikia mwaka 2030, kuongezeka wanufaika wa huduma kutoka 325,000 mpaka 1,009,548, kuongeza mtandao kutoka asilimia 44 mpaka asilimia 100 ambapo km 760.4 za mabomba zitalazwa.
Pia, kuongeza mtandao wa majitaka ulio asilimia 7.6 kwa sasa mpaka asilimia 30 ambapo km 192 za mabomba ya majitaka zitalazwa na kunufaisha wananchi 201,811, ujenzi wa mtambo mpya wa kutibu majitaka wenye uwezo wa kutibu lita milioni 22 za majitaka kwa siku pamoja na kujengea uwezo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) kupitia mafunzo, ununuzi wa samani za ofisi na vitendea kazi.
Waziri Aweso amemuhakikishia Bw. Cheptoo kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maji itazutumia fedha zinazotolewa kikamilifu kwa faida ya wananchi wote Tanzania waishio mijini na vijijini kuhakikisha wanapata huduma ya uhakika ya majisafi na salama.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Amos Cheptoo amesema lengo la ujio wao ni kujionea kazi iliyofanyika ya mradi wa jiji la Arusha na wataendelea kuipa ushirikiano Tanzania ili kuhakikisha Serikali inafikia malengo yake kwa upande wa Sekta ya Maji pamoja na sekta nyingine
Comments
Post a Comment